Posted by Esta Malibiche ON JUNE 30,2017 IN NEWS
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii ,Kanda ya Kaskazini.
ENEO
la njia Panda linalounganisha barabara za Moshi/Arusha,Tanga/Dar es
Salaam na ile ya Holili mpakani mwa nchi jirani ya Kenya linatajwa kama
kituo kikuu cha Malori yanayosafirisha Nafaka kwenda nchi jirani ya
Kenya.
Uchunguzi
uliofanywa na Globu ya Jamii umebaini kuwepo kwa maeneo yasiyo rasmi ya
kuegesha Malori hayo ,mengine yakiwa na Matela yake ,ambako shughuli za
kupakua mahindi na kupakia katika Magari Madogo aina ya fuso zinazotoka
nchi jirani ya Kenya hufanyika.
Maeneo mengine yanayotajwa kuwepo na Magulio ya Mahindi ni katika sehemu za maegesho ya magari zilizopo katika vituo mbalimbali vya kuuza Mafuta ,pamoja na baadhi ya nyumba za wageni ambazo zimegeuzwa Maghala ya kuhifadhia Mahindi.
Magari
zaidi ya 103 yanashikiiwa katika maeneo ya Njia Panda na Himo yakiwa
yamebeba Shehena ya Mahindi tayari kusafirishwa huku baadhi ya madereva
wakiyatelekeza Malori yao kwa siku ya tano sasa na kwenda kusiko
julikana .
Hatua
iliwasukuma Wafanyabiashara wa Mahindi pamoja na Madereva kufika ofisi
za Mkuu wa mkoa kuwasilisha malalamiko yao juu ya kukamatwa kwa Malori
hayo yakiwa Njia Panda badala ya mpakani kama alivyo agiza Waziri
Mkuu,Kassim Majaliwa.
Wakizungumza
nje ya jingo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Wafanyabiashara hao ,Laurance
Kanyota,Nuru Madai na Mariam Ramadhan walisema wameshangazwa na hatua ya
jeshi la Polisi kushikilia magari yao yalikuwa na Mahindi
yakisafirishwa kuelekea mikoa ya Arusha na Moshi.
“Magari
yetu yapo pale Sheli Maount Meru,yalitokea Tunduma kwenda
Arusha,yalipofika pale siku ya Jumamosi madereva walienda kula siku kuu
ya Idd,jana (Juzi) asubuhi Matandiboi
wakapiga simu kwamba tumezungukwa na Polisi ,tukaenda pale tukaonana na
OCD tukaliza kwanini mnatushikia magari ambayo yako Njia Panda
yanayoenda Arusha au Moshi ,wakajibu tumetumwa kushika magari yote ya
Mahindi.”alisema Mfanyabiashara Mariam.
Alisema alimuelewa Waziri Mkuu katika agizo lake kwamba magari yaliyopo mpakani ndio yashikiliwe na
si kama lilivyofanya jeshi la Polisi kukamata magari yaliyokuwa Njia
Panda kuelekea Moshi na Arusha huku wakimuomba Waziri Mkuu kutoa
ufafanuzi kwa wasaidizi wake juu ya agizo lake.
Mfanyabiashara
Kanyota alisema amekuwa akifanya biashara ya kusafirisha mazao kwa njia
halali ikiwa ni pamoja na ulipaji wa kodi lakini anashangazwa na hatua
ya kuzuiliwa kwa Mahindi yake ambayo amekuwa akinunua na kuyauza katika viwanda vya kutengeneza unga kwa ajili ya Chakula.
“Tulikua
tunaomba Mkuu wa mkoa ajue kwamba sisi ni wafanyabiashara tunaolipa
kodi halali ya serikali atusaidie tufikishe mazao yetu sehemu
yanapotakiwa kufika ,Mahindi yangu yanatoka Mbeya ,mkulima aiyeniletea
mimi kama Dalali ametoka Tunduma.”alisema Kanyota.
Kauli ya Serikali ya mkoa wa Kilimanjaro.
Kamati
ya ulinzi na usalama mkoa wa Kilimanjaro imepigiria msumari katika
Agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kutaifisha Mahindi pamoja na
gari litakalokutwa kuanzia June 26 mwka huu likiwa limebeba na
kusafirisha Mahindi kwenda nje ya nchi.
Mkuu wa mkoa wa Kilimajaro Anna Mghwira ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa alisema jana
ofisini kwake mbele ya waandishi wa habari kuwa magari 103 yaliyokamatwa
Himo na Njia Panda yatahesabiwa kama sehemu ya uhujumu uchumi na kwamba
yatataifishwa .
“Magari yaliyokamatwa kule Siha ,tayari tulikwisha amua kwamba yatapelekwa Nationa Milling(Ghala la chakula la taifa) Arusha
,lakini haya ya Himo ,Waziri Mkuu Alisha agiza kwamba kuanzia tarehe 26
,magari yote yatakayokamatwa ,Bidhaa pamoja na magari yenyewe
yatahesabiwa kuwa ni sehemu ya uhujumu Uchumi ,kwa hiyo
yatataifishwa.”alisema Mghwira.
Mghwira
alisema baada ya mfululizo wa vikao vya kamati ya ulinzi na usalama ya
mkoa wa Kilimanjaro juu swala zima la uuzaji na usafirishaji wa chakula
nje ya nchi,kamati imefanyia kazi tamko la Waziri Mkuu kutaka
kujiridhisha vya kutosha juu ya hali ya chakula iliyopo Kilimanjaro na
mikoa ya jirani.
“Uogozi
wa mkoa wa Kilimanjaro unapenda kuwatangazia wananchi wote,hususani
Wafanyabiashara wa Sukari na Nafaka za Mpunga,Mchele ,Mahindi na Unga wa
Mahindi ya kuwa ni marufuku kwa mfanyabiashara yoyote au mwananchi
yoyote kusafirisha bidhaa hizo kwenda nje ya nchi bila kibali cha
serikali”alisema Mkuu huyo wa Mkoa .
Alisema kukiuka agizo hilo ni kuhujumu uchumi wa nchi kama
ilivyo ainishwa kwenye kifungu cha 3 cha jedwali la kwanza la sheria ya
uhujumu Uchumi sura ya 200 ya sheria za Tanzania na pia ni kukiuka
agizo la Waziri Mkuu,kupitia waraka wake alioutoa Mei 30,2017,uliozuia utokaji wa vyakula na sukari kwenda nchi jirani .
Alisema
kwa kukiuka sheria hiyo kunaweza kusababisha upungufu wa chakula kwenye
baadhi ya maeneo nchini na kusababisha Mamlaka ya Mapato hapa nchini
(TRA) kukosa takwimu muhimu wa bidhaa zinazosafirishwa nje
“Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro imejiridhisha kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakisafirisha sukari na
nafaka hizo nyakati za usiku na hiki ndicho kinaleteleza kukosa takwimu
muhimu kwa kupitia njia ambazo si rasmi kwa kushirikiana na baadhi ya
askari polisi ambao sio waaminifu.
Wakati
wa baraza la Idd lilifanyika kitaifa katika msikiti wa Riadha mjini
Moshi,Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa alitangaza kupiga marufuku
usafirishaji wa Mahindi kwenda nchi jirani na kwamba atakaye kiuka
utaratibu huo atahukuliwa hatua kali za kisheria.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira akiwa ameongozana na baadhi ya
wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kilimanjaro wakiwemo
Kamanda wa Polisi ,Hamis Issah na Mkuu wa wilaya ya Moshi ,Kippi Warioba
wakitembelea maeneo ambayo yameshikiliwa magari yaliyobeba shehena ya
Mahindi .
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira akizunbgumza na baadhi ya
wafanyabaishara wa Mahindi ambao magari yao yanashikiliwa eneo la Njia
Panda mkoani Kilimanjaro.
Baadhi
ya Wafanyabiashara ambao Mahindi yao yanashikiliwa katika eneo la Njia
Panda mkoani Kilimanjaro wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna
Mghwira alipofika eneo hilo kwa lengo la kuzungumza nao.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira akiangalia magari yaliyobeba
shehena ya Mahindi yanayoshikiliwa katika eneo la Njia Panda ya Himo.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira akizungumza na baadhi ya madereva
na Wafanyabaisahara ambao Mahindi yao yanashikiliwa eneo la Njia Panda
ya Himo.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira akitizama Malori yenye Shehena ya
Mahindi yakiwa yamehifadhiwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyuma ya
vituo vya Mafuta .
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira akiongozana na Kamanda wa Polisi
mkoa wa Kilimanjaro,Hamis Issa wakiodoka katika eneo hilo baada ya
kuangalia malori yanayoshikiliwa yakiwa na shehena ya Mahindi.
Baadhi ya Magari yakiwa yameegeshwa katika maeneo tofauti tofauti yakiwa na shehena ya Mahindi.
0 maoni:
Chapisha Maoni