Ijumaa, 30 Juni 2017

MBUNGE ROSE TWEVE KUTUMIA ZAIDI YA MILIONI 60 KUSAIDIA WANAWAKE WA MKOA WA IRINGA

Posted by Esta Malibiche on JUNE 30,2017







MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Rose Tweve (CCM) amepanga kutumia zaidi ya Sh Milioni 60 kutoka katika mshahara wake kuwawezesha wanawake katika kata 107 za mkoa wa Iringa kuanzisha mifuko maalumu ya kuwezeshana kiuchumi.
Zaidi ya kata 40 za wilaya ya Iringa, Kilolo na Mufindi zimekwishanufaika na mpango huo unaokiwezesha kikundi cha wanawake katika kila kata kupata Sh 600,000 ambazo hazirudishwi.
Akikabidhi kiasi hicho cha fedha kwa vikundi vya kata za Nyololo na Malangali, Tweve alisema zoezi hilo litaendelea katika kata zingine zote zilizobaki zitakazokamilisha taratibu mbalimbali ikiwemo ya kuunda uongozi wake na kufungua akaunti benki.
Tweve alisema kwa kupitia mifuko hiyo itakayojulikana kama mifuko ya Rose Tweve ya kila kata wanawake watajiwekea utaratibu wa kuweka na kukopa, kuinuana kimaendeleo na kubuni mambo mengine yatakayowazidishia kasi ya maendeleo yao.
“Wanawake tupo wengi sana, lakini tunakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoturudisha nyuma. Huu ndio muda wa kujipanga upya na kubadili maisha yetu kwa kutumia kauli mbiu ya rais wetu Dk John Magufuli ya Hapa Kazi tu,” alisema.
Alisema kutakuwepo na utaratibu wa kuvifanyia tathimini vikundi hivyo na vile vitakavyofanya vizuri vitapata nyongeza ya fedha kila mwaka kwa kupitia mpango huo.
“Nimeanzisha mpango huu kwa kutumia rasilimali zangu mwenyewe na kwangu mimi naona hili la kusaidia wanawake wenzangu kwa kutumia rasilimali zangu linawezekana,” alisema.
Alisema matokeo chanya yatakayojitokeza  katika vikundi hivyo yatamshawishi atafute wafadhili wengine wa ndani na nje ili wasaidie zaidi.
“Sitoi fedha hizi ili mgawane kwa matumizi yasiofaa, natoa kama jitihada zangu za kuwahamasisheni kuona haja ya kuwekeza kwa pamoja na kwa manufaa ya wote,” alisema.
Alikipongeza kikundi cha kata ya Mtitu wilayani Kilolo ambacho mapema mwaka huu alikipatia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wake ambao sasa una zaidi ya Sh Milioni 1.8. 
Akishukuru kwa mchang huo, mmoja wa viongozi wa kikundi cha wanawake wa mfuko wa Rose Tweve wa kata ya Malangali, Judith Kisinini alisema wako katika mchakato wa kuanzisha duka la kuuza pembejeo za kilimo, hatua itakayowawezesha wanawake wakulima wa kata hiyo kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu.
Kisinini alisema kikundi chao chenye wanachama zaidi ya 200 hadi sasa kimejiwekea taratibu mbalimbali za kufikia malengo yao na kila mwaka kila mwanachama atalazimika kuchangia sh 50,000 kama hisa.
“Fedha hizo pamoja na michango ukiwemo wa mheshimiwa mbunge na faida tutakayokuwa tunapata kutoka katika shughuli tutakazokubaliana kufanya zitatumika kuendeleza wanachama wote bila ubaguzi wowote,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Nyololo, Grace Mbembati alisema; “mchango waliopata kutoka kwa mbunge huyo utatuongezea kasi katika kutimiza wajibu wetu ili kufikia azma tuliyonayo katika kusaidiana kiuchumi.”

Diwani wa kata ya Malangali ambaye pia ni katibu wa mbunge huyo, Shakila Salim aliunga mkono juhudi za mbunge huyo kwa kuvichangia vikundi hivyo Sh 100,000 kila kimoja.

0 maoni:

Chapisha Maoni