Posted by Esta Malibiche on JUNE 30,2017 IN NEWS.
Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Sileshi Bekele ( wa tatu kushoto) akieleza jambo katika ziara hiyo. |
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani ( wa pili kulia mbele)
akimwongoza Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk.
Seleshi Bekele (katikati mbele) kwenye ziara ya kukagua eneo la ujenzi
wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji la Stiegler’s
Gorge, Rufiji mkoani Pwani katika ziara hiyo.
Na Greyson Mwase, Rufiji.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani amesema Tanzania
inatarajia kupata umeme wa uhakika wa Megawati 5000 ifikapo mwaka 2021,
mara baada ya kukamilika kwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu
za maji katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji kwenye eneo la
Stiegler’s Gorge lililopo Rufiji mkoani Pwani ambao utaongeza umeme wa
kiasi cha Megawati 2100 katika gridi ya taifa.
Dk.
Kalemani aliyasema hayo jana tarehe 29 Juni, 2017 katika ziara ya Waziri
wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele
aliyeambatana na wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha
umeme kwa kutumia maji kutoka Ethiopia kwenye eneo la mradi wa
kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji ya
Stieglers Gorge wilyani Rufiji mkoani Pwani.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani akishuka kwenye boti kwa
ajili ya kuelekea kwenye eneo la Stieglers Gorge kutakapojengwa mradi
huo.
Wengine
walioshiriki katika ziara hiyo ni pamoja na wataalam wa masuala ya
umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania, Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini. Ziara hiyo inafuatia maombi
ya Rais John Magufuli kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia ya kutuma wataalam
wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za
maji kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na wataalam wa masuala ya umeme
na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania.
Dk
Kalemani alisema kuwa kupatikana kwa umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2021
kutachochea ongezeko la viwanda hivyo kuongezeka kwa fursa za ajira na
biashara na kukuza uchumi wa nchi.
Alisema
mradi huo mkubwa ni moja ya mikakati ya Serikali kuhakikisha nishati
inakuwa na mchango mkubwa katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo
ya Taifa yenye lengo la kuhakikisha kuwa nchi inatoka katika orodha ya
nchi maskini duniani na kuingia katika orodha ya nchi zenye uchumi wa
kati ifikapo mwaka 2025.
Waziri wa
Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele
(kushoto) akieleza jambo kwa Mhaidrolojia Mwandamizi kutoka Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO), Stanislaus Kizzy (kulia) katika ziara hiyo.
Anayesikiliza katikati ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard
Kalemani.
Alisisitiza
kuwa mbali na mradi huo mkubwa, serikali imeweka mikakati ya kutumia
vyanzo vingine vya nishati kama vile Gesi, Makaa ya Mawe, Jotoardhi,
Upepo ili kuhakikisha kuwa nchi inapata umeme wa uhakika. Akielezea
mafanikio ya mradi huo mbali na upatikanaji wa umeme wa uhakika, Dk.
Kalemani alisema kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa shughuli za uvuvi
katika mkoa wa Pwani.
Alitaja
mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kukuza sekta ya Utalii katika mkoa
wa Pwani pamoja na kuzuia mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa
mara katika mto Rufiji na kuathiri makazi ya wakazi waishio pembezoni
na mto huo. Akielezea hatua iliyofikiwa ya maandalizi ya ujenzi wa mradi
huo mkubwa, Dk. Kalemani alisema baada ya timu ya wataalam kutoka
Tanzania na Ethiopia kufanya ziara katika eneo la mradi hatua
inayofuatia ni wataalam kukaa vikao mbalimbali kujadili namna bora ya
kutekeleza mradi pamoja na kubadilishana uzoefu.
Mhaidrolojia
Mwandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Stanislaus Kizzy
(kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji
kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele ( wa pili kushoto). Katikati ni
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.
Alisema
mara baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika, moja ya kazi
zitakazofanywa ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme hadi
Chalinze yenye urefu wa kilomita 200 na njia ya kusafirisha umeme kutoka
eneo la Mradi hadi Singida yenye urefu wa kilometa 800.
Waziri
Kalemani aliwataka wananchi na taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi
za Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya
maji hususan katika mto Rufiji.
Wakati
huohuo, katika ziara hiyo Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji
kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele alisema kuwa mradi huu mkubwa ni
mzuri na unatekelezeka na kuongeza kuwa Ethiopia ipo tayari kutoa
ushirikiano mkubwa kupitia wataalam wake lengo likiwa ni kuhakikisha
kuwa mradi unafanikiwa na kukamilika kwa wakati.
Kaimu
Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga
(kulia) akipokewa na Meneja Mkuu wa Hoteli ya Serena Mivumo River Lodge,
Ellieta Mbisse (kushoto) mara bada ya kuwasili katika uwanja mdogo wa
Stiegler’s Gorge, Rufiji mkoani Pwani kabla ya kuanza kwa ziara ya
Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi
Bekele aliyeambatana na wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya
kuzalisha umeme kwa kutumia maji kutoka Ethiopia pamoja na wataalam wa
masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania wakiongozwa na
mwenyeji wao Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani akishuka kwenye
helikopta, mara bada ya kuwasili katika uwanja mdogo wa Stieglers
Gorge, Rufiji mkoani Pwani kabla ya kuanza kwa ziara ya Waziri wa Maji,
Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele
aliyeambatana na wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha
umeme kwa kutumia maji kutoka Ethiopia pamoja na wataalam wa masuala ya
umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania.
Kaimu
Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga
(kushoto) akielezea maandalizi ya mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia
nguvu za maji wa Stieglers Gorge kwa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya
Ethiopian Construction Design and Supervision kutoka Ethiopia, Dk.
Negede Kassa (kulia) katika ziara hiyo.
Kipimo cha kupimia kina cha maji (water gauge) katika sehemu ya mto Rufiji uliopo katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Sehemu
ya Mto Rufiji kutakapojengwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu
za maji katika eneo la Stieglers Gorge wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Waziri
wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele
(wa saba kulia) na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani
(wa nane kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya wataalam
kutoka Tanzania na Ethiopia katika ziara hiyo.
0 maoni:
Chapisha Maoni