Posted by Esta Maliobiche on JUNE 21,2017 IN NEWS
Jovina Bujulu-MAELEZO.
Hivi karibuni Serikali kupitia
Ofisi ya Waziri Mkuu imezindua programu ya kitaifa ya kukuza ujuzi wa
nguvu kazi wa stadi za maisha kwa vijana mkoani Iringa ikiwa ni
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 hadi
2020/2021.
Akiwasilisha hotuba kuhusu
mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na
matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge 2017/2018
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
(Mb) alisema kuwa kwa kutambua kuwa asilimia 56 ya nguvu kazi ya taifa
ni vijana, ndiyo maana imechukua jukumu la kutekeleza programu ya kukuza
ujuzi na stadi za kazi kwa vijana.
Madhumuni ya programu hiyo ni
kuwawezesha vijana kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda pamoja
na kuinua ari ya vijana kupenda kufanya kazi ili kuwaongezea kipato na
kuinua hali zao za maisha.
Awamu ya kwanza ya programu hiyo
itawanufaisha vijana wapatao 3,400 ambao watapata mafunzo ya stadi
mbalimbali ambazo zitawasaidia kujiajiri na kuajiriwa na hatimaye
kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
Akifungua mafunzo hayo, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye
Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa program hiyo inagharimiwa na
Serikali ya awamu ya tano kwa kushirikiana na Taasisi ya Wasalesiani wa
Don Bosco.
Alisema kuwa Serikali haitasita
kusitisha mkataba na taasisi hiyo endapo watagundua kuwa mafunzo
yanayotolewa hayatakuwa na viwango na ubora wanaohitaji.
Naye Padre Simon Akira aliahidi
kuwa watafanya vizuri na aliishukuru Serikali kwa kuatambua mchango wa
taasisi hiyo wa kuwahudumia vijana.
“Mpango huu ni sehemu ya kuwaandaa
vijana ambao watashiriki katika mapinduzi ya viwanda nchini na
utasaidia kutoa fursa kwa vijana kupata mafunzo ya uanagenzi katika
nyanja za ujenzi, TEHAMA, ufundi magari na ushonaji nguo” alisema Mhe.
Mhagama.
Aidha, alisema kuwa Serikali
imeweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya
uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Kwa sasa mwelekeo wa miaka
mitano 2016 hadi 2021 ni kujenga taifa lenye viwanda vya kuzalisha
biashara za kutosheleza mahitaji ya soko la ndani na kuuza nje ya nchi.
Ili kufikia azma hiyo, nguvukazi yenye ujuzi wa kutosha kumudu mahitaji ya soko la ajira ni muhimu iwepo.
Kutokana na umuhimu huo, Serikali
ilijumuisha programu hiyo ili kukuza ujuzi na nguvu kazi ya taifa
hususani vijana ili pamoja na kupata ujuzi ipunguze tatizo la ajira
nchini. Programu hiyo ya miaka mitano inahusisha vijana kutoka mikoa
yote nchini.
Katika utafiti wa nguvu kazi
uliofanyika 2014, unaonesha idadi kubwa ya nguvu kazi iliyokuwa kwenye
ajira takribani asilimia 79.9 ina kiwango cha chini cha ujuzi na
asilimia 16.6 ina kiwango cha kati cha ujuzi ambapo asilimia 3.6 ina
kiwango cha juu cha ujuzi.
“Ili kutufikisha katika uchumi wa
kipato cha kati, taifa linatakiwa kuwa angalau na asilimia 12 ya ujuzi
wa kiwango cha juu, asilimia 34 ya ujuzi wa kiwango cha kati na kutozidi
asilimia 54 kwa kiwango cha chini “ alisema Mhe. Mhagama.
Katika kuhakikisha mpango wa
maendeleo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 ,
Serikali kupitia programu hiyo inalenga ifikapo mwaka 2021 vijana
wapatao 100,000 wapate mafunzo kupitia programu za uanagenzi, kutoa
mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu 1,200,000 na kutoa mafunzo ya kuongeza
ujuzi kwa wafanyakazi 1,700,000.
Aidha, programu hiyo itatambua na
kurasimisha ujuzi uliopatikana wa vijana 1,000,000 walioajiriwa na
waliojiajiri ili kuziba nafasi hiyo ya ujuzi.
Mafunzo hayo pia ni maandalizi ya
kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na vijana wengi wenye sifa na stadi
za kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo viatu na nguo ili kuhakikisha
nchi inakuwa mstari wa mbele katika kutimiza makubaliano ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki ambayo ni kuachana na nguo na viatu vya mitumba ifikapo
2018.
Mafunzo hayo pia yanalenga
kuwaandaa vijana wengi wenye stadi mbalimbali na kuhakikisha kuwa
wanawezeshwa kufanya kazi katika viwanda vilivyopo na vitakavyojengwa.
Kwa upande wa sekta ya nguo na
viatu, vijana 3,000 wameanza kupata mafunzo kwa kubuni na kushona nguo
kwa kutumia teknolojia za kisasa kupitia kiwanda cha TOOKU kilichopo
jijini Dar es salaam na kiwanda cha MAZAVA cha mjini Morogoro.
Vijana wengine watapata mafunzo ya
kutengeneza bidhaa za ngozi ikiwemo viatu na pochi, uselemala, ufundi
uashi, ufundi magari, uchongaji vipuri, ufundi bomba, ufundi vyuma na
kuweka terazo na vigae.
Hakika taasisi ya Net Don Bosco
Tanzania kupitia Vyuo vyake nane nchini vitahusika kuwapatia mafunzo
vijana wengi zaidi nchini ili waweze kutoa mchango wao kwa familia zao
na taifa kwa ujumla.
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Anthony
Mavunde amesema kuwa programu hiyo ya miaka mitano ndiyo fursa ya ajira
pekee ya kumfanya kijana aweze kujiajiri na kuajiri vijana wenzake.
Waziri Mhagama alitoa wito kwa
viwanda na taasisi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushirikiana na
Serikali katika kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa vijana hao ili
kuwajengea umahiri wa stadi za kazi ili kuwawezesha vijana wenye ujuzi
bora kuajiriwa na kuwaajiri watakapohitajika.
Fursa hiyo adhimu kwa Vijana ni
muhimu, wanapaswa kuitumia kama njia itakayowapa mtaji waweze kujifunza
stadi mbalimbali na baadaye waunde vikundi na kufungua kampuni na
viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza bidhaa mbalimbali.
0 maoni:
Chapisha Maoni