Posted by Esta Malibiche on JUNE5,2017 IN NEWS
Na Jonas Kamaleki -MAELEZO
Vijana Wazalendo wamempongeza Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua
alizozichukua kuwapinga wanyonyaji wa uchumi na rasilimali za nchi
kupitia sekta ya Nishati na Madini.
Pongezi hizo zimetolewa leo jijini
Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wazalendo Tanzania, Bwana
Mwita Nyarukururu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Bwana Mwita amesema ana hakika
kuwa Watanzania wanafuatilia juhudi za Mhe. Rais Magufuli katika sekta
ya Nishati na Madini kwa kuunda Tume ya wataalam mbalimbali kufanya
uchunguzi na upembuzi yakinifu katika madini.
“Wote tumeshuhudia ripoti ya
wataalam wa madini chini ya Mwenyekiti, Prof. Abdulkadir Mruma ambapo
Tume imeeleza masikitiko yake makubwa dhidi ya makampuni ya madini
nchini yanavyokwapua na kusafirisha raslimali zetu bila Taifa
kunufaika”, alisema Mwita
Aidha, Mwita amesema kuwa
unyonyaji na uhujumu uchumi katika sekta ya madini umekuwa ukipigiwa
kelele kwa takriban miaka 17 na wazee pamoja na wananchi kwa ujumla juu
ya tahadhari yao kwa Taifa kuwekeza katika uzalishaji wa madini kutokana
na mikataba kuwa ya siri na mibovu isiyonufaisha wananchi.
Aidha wamemwomba Mhe. Rais kuvunja
mikataba ambayo haina maslahi kwa taifa bila kujali udogo au ukubwa wa
kampuni hizo, ikiwa ni pamoja na kupeleka Bungeni mikataba na sheria
zote zinazohusu nishati na madini kwa lengo la kujadiliwa upya kwa
maslahi mapana ya Taifa .
Kwa upande wake, mjumbe wa Jukwaa
la Wazalendo, Bi. Rose Manumba amesema inashangaza kuona huduma za
kijamii kama sekta ya Afya, Elimu na Miundombinu zinazorota kwa kukosa
fedha wakati matrililioni ya fedha yanachukuliwa na wajanja wachache.
Amemuomba Mhe. Rais na wananchi
kwa ujumla wasichoke katika mapambano haya ya kukomesha wizi wa
raslimali za Watanzania walizopewa na Mungu.
“Kwa kweli tumuunge mkono
Mheshimiwa Rais katika vita hii ili nchi yetu na raslimali zake ziwe na
manufaa kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo”, alisema Manumba.
Mwezi uliopita Mhe. Rais alipokea
Ripoti ya uchunguzi wa Makinikila ambayo ilionyesha kuwa tani za dhahabu
na madini mengine yenye thamani kubwa yalipatikana kwenye mchanga
uliokuwa usafirishwe nje ya nchi. Katika ripoti hiyo jumla ya takriban
tani 15 za madini zilikutwa kwenye makontena 277 ya makinikila
yayozuiliwa kusafirishwa nje na Mhe. Rais Magufuli, thamani yake
inakadiriwa kuwa ni shilingi za Kitanzania trililioni 1.3.
Kufuatia ripoti hiyo, uteuzi wa
Waziri mwenye dhamna ya Nishati na Madini, Prof. Sospiter Muhongo
ulitenguliwa na Mhe. Rais, na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Madini Nchini, alisimamishwa kazi.
Juhudi hizi za Mhe. Rais katika kupambana na ufisadi nchini zimeungwa mkono na watanzania wengi wakiwemo viongozi wa dini.
0 maoni:
Chapisha Maoni