Ijumaa, 30 Juni 2017

KOROSHO MKOANI SINGIDA KUWA ZAO LA KIBIASHARA NA LA KUDUMU.

Posted by Esta Malibiche on JUNE 30,2017 IN NEWS

unnamed
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Amour Hamad Amour akipanda Mkorosho katika eneo la shule ya Msingi Kipumbuiko, Wilayani Ikungi katika uzinduzi wa upandaji mikorosho kimkoa.
1
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Amour Hamad Amour akiweka chupa ya maji iliyofungwa na kutobolewa tundu dogo litakalokuwa likimwagilia kwa matone Mkorosho alioupanda katika eneo la shule ya Msingi Kipumbuiko, Wilayani Ikungi ambapo maji ya chupa hiyo yataisha baada ya siku nne katika uzinduzi wa upandaji mikorosho kimkoa.
2
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Amour Hamad Amour akielekezwa na Afisa Kilimo Kijiji cha Kipumbuiko Esther Bayda namna ya kuuwekea kivuli mche wa mkorosho alioupanda ili kutunza unyevu unyevu katika eneo la shule ya Msingi Kipumbuiko, Wilayani Ikungi katika uzinduzi wa upandaji mikorosho kimkoa.
3
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Amour Hamad Amour akizindua upandaji mikorosho kimkoa katika eneo la shule ya Msingi Kipumbuiko Wilayani Ikungi, akishuhudiwa na Mkuu wa Wiaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu (kulia kwake) na Mkimbiza mwenge Kitaifa Fredrick Ndahani (kushoto kwake).
4
Mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa Fredrick Ndahani akiuwekea kivuli mche wa mkorosho alioupanda ili kutunza unyevu unyevu katika eneo la shule ya Msingi Kipumbuiko, Wilayani Ikungi katika uzinduzi wa upandaji mikorosho kimkoa
5
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Amour Hamad Amour akikagua shamba la Mikorosho katika eneo la shule ya Msingi Kipumbuiko, Wilayani Ikungi katika uzinduzi wa upandaji mikorosho kimkoa pembeni yake Afisa Kilimo Kijiji cha Kipumbuiko Esther Bayda na nyuma yake ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu.
………………………….
Halmashauri za Mkoa wa Singida zimetakiwa kusimamia taasisi za serikali zilizopo kwenye maeneo yao pamoja na wananchi wao wanapanda zao la Korosho ili kuhifadhi mazingira, kuongeza kipato na kutimiza azma ya kuwa zao la kudumu na la mda mrefu la kibiashara mkoani hapa.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Amour Hamad Amour ametoa maelekezo hayo wakati mwenge wa uhuru ukizindua upandaji wa zao la korosho kimkoa uliofanyika katika kijiji cha Kipumbuiko, Wilayani Ikungi ambapo wakimbiza mwenge kitaifa wameshiriki upandaji miche ya mikorosho.
Kabla ya kutoa maelekezo hayo Amour amekagua shamba la korosho la ukubwa wa ekari moja na miche 28 linalomilikiwa na shule ya msingi Kipumbuiko na kuelekeza kuwa upandaji mikorosho usiishie hapo bali kila taasisi yenye eneo inapaswa kupanda mikorosho ya kutosha.
“Leo tumezindua upandaji mikorosho kimkoa, sasa juhudi hizi zisiishie hapa, Mkurugenzi wa halmashauri ya Ikungi hakikisha kila taasisi inalima mikorosho ya kutosha ili lengo la kutunza mazingiza liweze kutimia kwa ufanisi” amesema na kuongeza kuwa
“Tunapoelekea kwenye Tanzania ya Viwanda tunapaswa kuongeza uzalishaji wa malighafi za kuhudumia viwanda vyetu, hivyo basi hamasisheni wananchi wapande mikorosho kwa wingi, hata mimi nimehamasika na lazima nitalima mikorosho”
Naye Mkimbiza Mwenge Kitaifa Fredrick Ndahani amesema zao la korosho limekuwa mkombozi wa uchumi kwa wananchi wa mikoa ya lindi na mtwara ambako wanaifananisha na dhahabu ya kijani, hivyo basi mkoa wa Singida unapaswa kusimamia zao hilo lenye manufaa makubwa.
Ndahani amesema korosho ni zao ambalo huweza kutumia maji kwa ufanisi kwakuwa inaweza kupandwa hata kipindi ambapo sio cha mvua nyingi na pia ni zao ambalo huweza kupandwa katika shamba ambalo lina mazao mengine.
Ameongeza kuwa wananchi Mkoani Singida wanapaswa kuchangamkia kilimo cha korosho kwakuwa mavuno yake ni endelevu huku akiwasisitiza kuwatumia na kuwapa ushirikiao  wataalamu wa taasisi zinazofanya tafiti na kutoa elimu ya kilimo cha Korosho.
Kwa upande wake mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kipumbuiko Mariam Makera amesema wanafunzi na wananchi wa kijiji hicho kwa kushirikiana na Wilaya ya Ikungi wameanzisha kilimo cha korosho shuleni hapo ili wananfunzi wajifunze kilimo hicho kwa vitendo na kuwahamasisha wazazi wao.
Makera amesema korosho zinazolimwa shambani hapo zimetumia teknolojia ya umwagiliaji maji kwa njia rahisi ya matone ambayo hutumia maji kwa ufanisi wa hali ya juu.
Zao la korosho Mkoani Singida limeanza kulimwa mwaka 1970 huku uendelezaji wake kwa Wilaya ya Ikungi ukianza mwaka 2013 ambapo hadi sasa mikorosho 17,000 imeshapandwa na lengo la upandaji mikorosho mingine kwa msimu wa mwaka 2017/2018 likiwa mikorosho laki tano.

0 maoni:

Chapisha Maoni