Alhamisi, 19 Aprili 2018

TIMU YA WANAWAKE SEKTA YA UCHUKUZI YAIBUKA KIDEDEA KOMBE LA MEI MOSI MKOANI IRINGA

Posted by Esta Malibiche on April 19,2018 in MICHEZO


Timu ya wanawake na kamba ya Uchukuzi wakiwavuta Tanesco (hawapo pichani) katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana   uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege. Uchukuzi ambao ni mabingwa watetezi wameshinda kwa mivuto 2-0. PICHA NA BAHATI MOLELI TAA




MKURUGENZI wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Bi. Easter Kazenga amezipongeza timu za sekta hiyo kwa kufanya vizuri katika  mashindano ya Kombe la Mei Mosi yanoyoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Iringa.
Bi. Kazenga amezipongeza timu za michezo ya kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume, soka, netiboli, karata, bao, draft, riadha na baiskeli za Uchukuzi baada ya kuwatembelea kwenye kambi yao mara baada ya kumalizika kwa michezo.
“Ninawapongezeni sana kwa kufanya vizuri katika michezo hii, nimekuja kuungana nanyi ili kuwatia moyo na nitakuwa hapa kwa siku kadhaa na baadaye Katibu Mkuu na wengine watakuja, hivyo tuendeleze ushindi na tuchukue vikombe vyote vya ubingwa,” amesema Bi. Kazenga.
Hatahivyo, amewasisitizia wachezaji hao kuwa na nidhamu wawapo ndani na nje ya kiwanja ili kujenga sifa nzuri ya sekta hiyo.
Uchukuzi SC inayoundwa na wachezaji wazoefu akiwemo aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Eliutely Mholeli alipata bao lake pekee kwa njia ya penati iliyofungwa na Mahamudu Khamis katika dakika ya 52 baada ya Sigfrid Kikoti kuchezewa rafu na Joseph Mlimi wa TRA.
Hatahivyo, wachezaji wa pande zote mbili walishindwa kuonesha mchezo mzuri kutokana na kucheza huku mvua ikinyesha na uwanja kujaa maji katika baadhi ya sehemu na kusababisha wachezaji kuanguka hovyo huku mpira ukikwama katika madimbwi.
Katika mchezo wa netiboli uliochezwa kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUKU), timu ya Uchukuzi iliwaadhibu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuwafunga magoli 38-13.
Uchukuzi SC inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa na Bandari, Judith Ilunda ilikwenda mapumziko wakiwa na magoli 15-7, ambapo hadi mwisho wa mchezo mfungaji wake Matalena Mhagama alifunga magoli 28 na Bahati Herman magoli 10, wakati wa Tanesco Tina Mbuisa magoli tisa na Caltace Manapo magoli manne.
Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya Msingi Mlandege, mabingwa watetezi timu ya Uchukuzi iliwavuta Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa mivuto 2-0.
Kwa upande wa wanaume mabingwa watetezi Uchukuzi waliwapeleka puta Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwavuta mivuto 2-0.

 
 Mchezaji wa timu ya wanawake ya Tanesco, Tina Mbusa akiongoza jahazi la Tanesco katika mchezo wa kuvuta kamba dhidi ya Uchukuzi, uliofanyika jana   Uwanja wa Mlandege. Uchukuzi walishinda kwa kuvuta mivuto 2-0.



Timu ya Wanaume ya Uchukuzi (kulia) wakiwavuta TRA katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege. Uchukuzi ambao ni mabingwa watetezi walivuta  mivuto 2-0.

Winga Pendo Rungu wa Tanesco (WA) akidaka mpira uliorushwa na Shaila Mhava (C) huku Neema Makassy (WD) na Subira Jumanne (C-jezi nyeusi) wa Uchukuzi wakijiandaa kuokoa hatari iliyokuwa ikielekezwa kwenye lango lao katika mchezo wa Mei Mosi uliofanyika jana  uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUKU) Iringa.

Winga Omari Kitambo (5) wa Uchukuzi akizongwa na beki Joseph Mlimi (2) wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mchezo wa michuao ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika  jana uwanja wa Samora mkoani Iringa. Uchukuzi walishinda ba 1-0


Kipa Frank Mvula wa timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akiwa ameshindwa kucheza mpira wa penati uliopigwa na Mahamudu Khamis wa Uchukuzi katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Samora. Uchukuzi walishinda bao 1-0.



Kipa Frank Mvula wa timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akiwa ameshindwa kudaka mpira wa penati uliopigwa na Mahamudu Khamis wa Uchukuzi katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Samora. Uchukuzi walishinda bao 1-0.




Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Bi Easter Kazenga (aliyevaa suti ya michezo rangi ya kijivu katikati mbele), jana akiwa na kikosi cha wachezaji wa michezo mbalimbali ya timu ya Uchukuzi inayoshiriki katika michuano ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika mkoani Iringa.

0 maoni:

Chapisha Maoni