Jumamosi, 21 Aprili 2018

BUNGE LAPITISHA BILLIONI 898 BAJETI YA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO.

Na Mwandishi Wetu Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia na kupitisha jumla ya Shillingi Billioni 898 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Wakijibu hoja mbalimbali za wabunge kuhusu Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amesema Wizara itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Ukatili wa kijinsia ikiwemo kutoa elimu kwa wazazi ili wawafundishe watoto wao.
Pia Mhe. Ummy Mwalimu amesisitiza kuwa kwa somo la elimu ya uzazi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuwapa uelewa wanafunzi ili waweze kujikinga na kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali imefanya uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini kwa kuyahakiki na kuyafuta Mashirika yote ambayo yamekosa sifa na kutofuata utaratibu na Sheria za nchi.
Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa huduma kwa wazee nchini kwa kuboresha makazi ya kulea wazee wasiojiweza, kuanzisha na kuratibu  madirisha maalum ya kutoa huduma za afya kwa wazee katika hospitali na kutoa kadi za matibabu kwa wazee hao.    
Bunge limepitisha Bajeti hii ikiwa imejumuisha fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida na matumizi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

0 maoni:

Chapisha Maoni