Jumamosi, 21 Aprili 2018

TIMU ZA NETIBOLI,KAMBA ZA UCHUKUZI ZANG'ARA KOMBE LA MEI MOSI KITAIFA MKOANI IRINGA

Posted by Esta Malibiche on April 21,2018 IN MICHEZO



Mchezji Mary Kajigiri (mwenye mpira) akiruka juu kudaka mpira katikati ya wachezaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika mchezo wa netiboli uliofanyika jana kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) mkoani Iringa

Mwadawa Hamis (GK-njano) akiuwahi mpira uliorushwa na Subira Jumanne (WD-njano) katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) mkoani Iringa

Mfungaji Matalena Mhagama (GS-Njano) akiwahi mpira uliorushwa na Mary Kajigili (-katikati) huku mlinzi Upendo Manjuu (GK-nyekundu) akitaka kuuwahi katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) Mkoani Iringa.

Mchezaji Eliza Dominick (C-nyekundu) akirusha mpira kwa Laurencia Mtui (GA-wa kwanza kushoto), huku Bahati Herman (GA-katikati) wa Uchukuzi akiwania mpira huo, katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) mkoani Iringa
Mchezaji wa timu ya netiboli ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Neema Mbuja (aliyenyoosha kidole mbele) akiwasisitiza jambo wachezaji wake wa kuvuta kamba wanaume walipokuwa wakivutana na Ukaguzi (NAO), katika mchezo wa michuano ya Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege mkoani Iringa
Wachezaji wa timu ya wanaume ya Uchukuzi (kushoto) wakiwavuta Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa mivuto 2-0 katika mchezo michuano ya  Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege mkoani Iringa.



Timu ya wanawake ya MUHAS (kulia) wakivutwa na Uchukuzi kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa kombe la michuano ya Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege mkoani Iringa. 

Timu  ya Ukaguzi (kushoto) wakiwavuta kwa taabu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa mvuto 1-0, mvuto wa pili walitoka sare ya 0-0, katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mlandege mkoani Iringa.


TIMU za michezo ya netiboli na kamba za Uchukuzi jana ziliendelea kung’ara kwa kushinda michezo yake katika michuano ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika kwenye viwanja mbalimbali mkoani Iringa.


Timu ya netiboli ya Uchukuzi inayoundwa na wachezaji wazoefu waliowahi kuchezea timu ya Taifa ‘Taifa Queens’ iliwapeleka puta na kuwafunga bila huruma Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa magoli 61-3.


Washindi wakiongozwa na mfungaji wake mahiri Matalena Mhagama aliyepachika magoli 40 na Bahati Herman magoli 20, na Fatma Namalechi aliyeingia kipindi cha pili kupachika goli moja waliipeleka Uchukuzi mapumziko ikiwa na magoli 32-3, wakati NCAA alipata magoli hayo matatu kupitia kwa Laurencia Mtui.


Katika mchezo wa kuvuta kamba wanaume timu ya Uchukuzi iliwavuta Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa mivuto 2-0, huku wanawake wakiwaadhibu MUHAS kwa mivuto 2-0, na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.


Timu ya wanawake RAS Iringa iliwavuta MUHAS kwa mivuto 2-0; huku wanaume ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ilivutwa kwa tabu Ukaguzi (NAO) kwa mvuto 1-0. Mvuto wa pili walitoka sare ya 0-0.  


Katika hatua nyingine mabingwa watetezi kwa upande wa soka, timu ya GGM inayoongozwa na wachezaji wenye uzoefu na waliokaa kwa muda mrefu pamoja, walishindwa kufurukuta mbele ya NAO ingawa wachezaji wake walijitahidi kufanya mashambulizi ya kushtukiza lakini hadi mchezo unamalizika walitoka sare ya 0-0.


Katika netiboli timu ya RAS Iringa juzi iliwaadhibu bila huruma Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kuwafunga magoli 54-3 katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) mkoani Iringa. Washindi walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 29-3.


Wakati huo huo, leo wachezaji wa mchezo wa baiskeli leo watachuana kwa upande wa wanaume kilometa 35 zitakazoanzia kwenye mizani ya Ndolela na kumalizia eneo la FFU. Wanawake watachuana kilomedta 20.







0 maoni:

Chapisha Maoni