Posted by Esta Malibiche on April 21,2018 in NEWS
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza wakati alipoweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa
magahala na vihenge vya kisasa katika eneo la Kizota mjini Dodoma
Aprili 21, 2018.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
…………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini imeimarika na
kufikia tani milioni 15.9 kwa msimu wa mwaka 2016/2017 na 2017/2018 sawa
na kuwa na ziada ya tani milioni 2.6.
Pia Serikali ya Awamu ya Tano
inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa kuiwezesha Wizara ya Kilimo
kuongeza uwezo wa hifadhi ya Taifa ya chakula kutoka tani 251,000 za
sasa hadi tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumamosi, Aprili 21, 2018) wakati akiweka jiwe la msingi kwenye Mradi
wa Ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa vya kuhifadhia chakula,
Kizota mjini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema mkakati huo
utahusisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo ili kuongeza
thamani ya mazao kabla ya kuuzwa nje ya nchi na hivyo kutoa fursa za
ajira na kuwaongezea kipato wananchi.
Amesema Serikali imefungua mipaka
na inaendelea na jitihada za kutafuta masoko ya nje pamoja na kuboresha
miundombinu ya kuhifadhi chakula kwa kujenga maghala na vihenge vya
kisasa katika maeneo mengine yenye uzalishaji mkubwa wa chakula.
Pia Waziri Mkuu amewasihi wananchi
watumia fursa za kiuchumi kwenye maeneo ambayo mradi huo utatekelezwa
kwa lengo la kuboresha na kuinua hali zao za maisha, hivyo watakuwa na
uwezo wa kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema Serikali imewekeza fedha
nyingi kwenye mradi huo mkubwa na baada ya kukamilika utakuwa na faida
kubwa kwa Taifa, hivyo amewataka viongozi wa NFRA wahakikishe kwamba
hakuna mahindi yatayoharibika katika maghala yao.
”Mikakati ya Serikali ni
kuhakikisha NFRA inakuwa na uwezo wa kuhifadhi akiba ya kutosha ya
chakula kwa ajili ya dharula lakini pia kuweka mazingira rafiki ya
kuwezesha wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao nje ya nchi bila
vikwazo”.
Hata hivyp, Waziri Mkuu ameziagiza
Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Mipango na Wakuu wa Mikoa ambayo
mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe
wanatimiza wajibu wao ili mradi ukamilike kwa wakati.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa
NFRA Bibi Vumilia Zikankuba alisema mradi huo unatekelezwa katika maeneo
manane ya Kanda za Wakala huo ambayo ni Dodoma (Dodoma), Mpanda
(Katavi), Songea (Ruvuma), Makambako (Njombe), Mbozi (Songwe),
Sumbawanga (Rukwa), Shinyanga (Shinyanga), Babati (Manyara).
Bibi Vumilia alisema katika Kanda
ya Dodoma wanajenga vihenge vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na
kufanya kanda hiyo kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 59,000 kutoka uwezo
wa sasa wa tani 39,000.
Alisema Serikali ya Tanzania na
Serikali ya Poland zilisaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu Septemba
2015 wa Dola milioni 55 sawa na sh. bilioni 124, kwa ajili ya ujenzi wa
mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi ya chakula.
“Utekelezaji wa mikataba kati ya
NFRA na wakandarasi ulianza Desemba 2017 ambapo muda wa utekelezaji ni
miezi 18 tangu tarehe rasmi ya kuanza utekelezaji wa mikataba ya
wakandarasi, hivyo kabla ya 2020 utakuwa umekamilika”.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Spika
wa Bunge Job Ndugai , Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye
Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama.
Wengine ni Naibu Waziri Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi na Ajira, Anthon Mavunde,
Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya na
Balozi wa Poland nchini Tanzania, Balozi Krzysztof Buzalski.
0 maoni:
Chapisha Maoni