Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akijadiliana jambo na Waziri wa Nishati Dk.Medard Kalemani wakiwa kwenye kijiji cha Nkunikhana .
Mkuu wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu akizungumza wakati akimkaribisha Waziri wa Nishati Dk.Medard Kalemani kuongea na wananchi kabla ya kuzindua uwashaji wa umeme kijiji cha Nkuninkhana wilayani humo.
Mbunge wa Singida Magharibi Elibariki Kingu akitoa salaam kabla Waziri wa Nishati Dk.Medard Kalemani hajazungumza na wananchi wa kijiji cha Nkhuninkana.
Wanachi wa kijiji cha Nkhuninkana wakionyesha furaha yao baada ya kuelezewa neema ya umeme katika kijiji chao.
..............................................................
WAZIRI wa
Nishati Dk.Medard Kalemani amefanya ziara na kukagua miradi ya umeme
iliyopo wilayani Ikungi mkoani Singida huku akiwasisitiza wakandarasi
kumaliza miradi kabla ya muda uliowekwa ili kuweza kujitathimini kabla
ya mkataba kuisha.
Dk. Kalemani
amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk.John Pombe Magufuli
imedhamiria kufikisha umeme kila kijiji na kitongoji hivyo wakandarasi
wanapaswa kuunga mkono dhamira hiyo kwa kufanya kazi kwa uadilifu.
“Pamoja na
kuwasisitiza,niwapongeze pia wakandarasi mnaoendelea kujenga miundombinu
ya umeme,nilishawapa maelekezo ya kuwasha umeme vijiji vitatu kila wiki
na leo tutawasha kijiji cha Ikungi Utaho, Nkhuninkana na
Kipumbuiko,”alisema Dk.Kalemani.
Amesema
serikali imetoa shilingi bilioni 15 kwa ajili ya miradi ya umeme nchi
nzima na umeme ni wakutosha baada ya kuzindua mitambo ya Kinyerezi
ambapo kwa sasa kuna ziada ya megawati 194.
“Maombi
yaliyotolewa na mkuu wa wilaya yenu Miraji Mtaturu na ya mbunge wa
Singida Magharibi Elibariki Kingu nimeyasikia na nitayazingatia kwa kuwa
viongozi hawa wanasimamia maendeleo ya wananchi vizuri sana,nielekeze
tu umeme ukifika kwenye kijiji ufike na kwenye vitongoji vyake na kila
nyumba itawekewa umeme,
“Mkoa huu wa
Singida REA awamu ya tatu kwa sehemu ya kwanza utavifikia vijiji 150 na
kubakiza vijiji 72 tu ambavyo vitamaliziwa na sehemu ya pili na ya tatu
ya REA awamu ya tatu kufikia mwaka 2021 hivyo nawaomba wananchi mtumie
fursa hii adimu kujiinua kiuchumi,”alisema Dk. kalemani.
Amesema
msingi wa kufanya yote hayo ni kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM 2015
-2020 katika kuwaletea wananchi Maendeleo na hasa kufikia Tanzania ya
Viwanda.
Akisoma
taarifa mbele ya dokta Kalemani,meneja wa Shirika la Umeme
Nchini(TANESCO)mkoa wa Singida mhandisi Abdulrahman Nyenye ameeleza kuwa
Mkoa umeendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme kupitia Mradi wa
umeme vijijini (REA )na kwamba REA awamu ya Pili ilianza novemba 25
mwaka 2013 hadi novemba 24 mwaka 2015 na ilitarajiwa kufikia vijiji 88
na kuunganisha wateja 8,332.
“Katika
awamu hiyo vilitakiwa vijiji 88 ila vilivyounganishwa ni vijiji 35 mpaka
sasa hii ni kutokana na mkandarasi kutokuzingatia mkataba na
alishaondolewa na kupatikana mkandarasi mwingine,na kwa sasa mradi wa
BACKBONE unaendelea katika mkoa wa Singida ambapo vijiji 39 vitapatiwa
umeme,”alisema meneja huyo.
Kwa upande
wake Mkuu wa wilaya Mtaturu amempongeza dokta Kalemani kwa kazi nzuri
anayofanya ya kuzunguka nchini kuangalia utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya umeme jambo linalodhihirisha namna anavyomuwakilisha mh
Rais vizuri.
“Pamoja na
pongezi hizo kwako sisi wakazi wa Ikungi tunakuomba utupelekee shukrani
zetu kwa mhe Rais kwa kutuweka kwenye mpango wa miradi ya REA mwaka huu
kwa mara ya kwanza ambapo vijiji 41 vitaunganishwa kwenye umeme ikiwa
ni pamoja na vijiji 11 vya backbone,
"Hii ni
historia mpya inaandikwa kwa kupata umeme toka nchi
imeumbwa,nikuhakikishie mh waziri umeme huu utatusaidia kuchochea uchumi
wa wananchi wetu,kwa sasa mkoa wetu tupo kwenye mkakati wa kuhakikisha
tunajenga viwanda ili kuunga mkono juhudi za mhe Rais kuifikia Tanzania
ya Viwanda na Uchumi wa kati kwa kuchakata mazao ya kilimo kama alizeti
na viazi,mifugo na kuweka kiwanda cha chumvi bonde la Misughaa na hivyo
kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya wakulima.,”aliongeza Mtaturu.
Amesema kwa
kuwa sasa wanapata umeme vijiji 41 kati ya 101 wanaomba REA awamu ya
tatu iunganishwe kwa pamoja ili kuvifikishia umeme vijiji vyote mapema
na kuyaweka kwenye mpango kwa sasa maeneo yanayohitaji umeme kwa
umuhimu wake kwa ajili ya kuvuta maji kwa wananchi kama
Matongo,Ulyampiti, Ihanja na Kimbwi.
Naye, Mbunge
Kingu amempongeza Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya ya kumsaidia Rais
kwenye Sekta ya Nishati na kuomba vijiji vilivyosahaulika katika eneo la
jimbo lake viingizwe kwenye mpango.
“Pamoja na
pongezi kwako nimpongeze pia mkuu wa wilaya yetu Mtaturu kwa kusimamia
vizuri Maendeleo ya wananchi wa Ikungi,na kutokana na kazi nzuri hii
mkuu wa wilaya nakukabidhi shilingi laki 400,000 hii ikiwa ni mchango
wangu kwa wananchi katika kuwasaidia gharama za kuweka umeme,hapa ni
shilingi 5,000 kwa kaya 80,”alisema kingu.
0 maoni:
Chapisha Maoni