Alhamisi, 14 Desemba 2017

RAIS DKT. MAGUFULI AFUNGUA MKUTANO MKUU WA CHAMA CHA WALIMU TANZANIA (CWT) MKOANI DODOMA

Posted by Esta Malibiche on DEC 14,2017 IN NEWS

1
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na mamia ya wanachama wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kabla ya kufungua mkutano huo  Mkuu wa (CWT )katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma. Wanachama hao wa CWT walisimama na kushangilia  mara baada ya ahadi ya Rais Dkt. Magufuli kuwaahidi kuendelea kutatua kero zao mbalimbali.


: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi kulipa madeni ya walimu takribani shilingi Bil. 25 mara baada ya  viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuthibitisha uhalali wa madeni hayo.
Rais Dkt. Magufuli ametoa tamko hilo leo Mjini Dodoma ,alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa CWT ambao umehusisha wawakilishi kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara   .
“Ninawaahidi walimu wenzangu, mara baada ya zoezi la uhakiki kuisha wale walimu ambao wanadai malipo halali watalipwa,” alifafanua Rais Dkt. Magufuli.
Aliendelea kusema kuwa kabla hajawa Rais alikuwa mwalimu hivyo anazifahamu vizuri shida za walimu hivyo walimu wajisikie wana muwakilishi mzuri.
Aidha, Rais Magufuli amewataka viongozi wa CWT wa wilaya na mikoa kuhakiki madeni ya walimu ya maeneo yao na kuyawasilisha kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kulipwa.
Rais Dkt. Magufuli amesema Serikali ya awamu ya Tano imeendelea kufanya jitihada za kuboresha maslahi ya walimu ambapo tangu imeingia madarakani jumla ya shilingi bilioni  56.92 zimetolewa kwa ajili ya kulipa madeni ya walimu ambapo kati ya fedha hizop, shilingi bilioni 14.23 ni madeni ya mishahara na shilingi  bilioni 42.69  ni madeni yasiyo ya mishahara.
Vile vile Rais Magufuli amewasihi walimu wenzake kupokea kile kidogo ambacho Serikali inakitoa wakati huu ambapo Serikali inawekeza katika kutekeleza miradi mbalimbali kama vile miradi ya afya, umeme, maji, barabara na reli. Miradi ambayo inawagusa pia walimu katika maisha yao ya kila siku nawanapotimiza majukumu yao.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amewaahidi walimu hao kufanyia kazi maombi mbalimbali ambayo wamewasilisha ikiwemo kurudisha posho ya kufundishia pamoja na  Serikali kutoa mikopo isiyo na riba ili kuwasaidia kujenga nyumba za kuishi.
Hata hivyo, amewata viongozi husika kushughulikia uwiano sahihi wa walimu wa shule za msingi na sekondari walioko mijini na vijijini kutokana na walimu wengi kupangiwa mijini.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais CWT Leah Ulaya amesema kuwa wanaimani na Rais Magufuli na juhudi zake zinaonekana wazi katika  kupambana na ufisadi, uzembe, rushwa, uhujumu uchumi na vita dhidi ya madawa ya kulevya.

4
Mamia ya Wajumbe wa Chama cha Walimu(CWT) wakishangilia ndani ya ukumbi wa Chimwaga wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akijibu kero zao mbalimbali walizoziwasilisha.
5
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na baadhi ya wajumbe wa Chama cha Walimu CWT mara baada ya kuwahutubia katika ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
6
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ameshikana mikono na viongozi wa muda wa  CWT,
Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako, Spika wa Bunge Job Ndugai, pamoja na mke wa Rais Mama Janeth Magufuli wakiimba wimbo wa mshikamano pamoja na Wajumbe wote wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) katika ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
7
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wakiwa wameshikana mikono wakati wakiimba wimbo wa mshikamano kabla ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuhutubia na kufungua mkutano huo wa CWT katika ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
9
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwasalimia wajumbe wa CWT katika ukumbi wa Chimwaga.
13
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwasikiliza viongozi wa muda wa Chama cha Walimu Tanzania walipokuwa wakiwasilisha hoja zao mbalimbali zinazo wakabili walimu nchini katika mkutano mkuu wa CWT uliofanyika katika ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
PICHA NA IKULU

0 maoni:

Chapisha Maoni