Jumatano, 13 Desemba 2017

RAIS MAGUFULI AREJESHA EKARI 129 KWA WANANCHI WA IYUMBU,DODOMA MJINI KUFUATIA MAOMBI YA MBUNGE MAVUNDE

Posted by Esta Malibiche on DEC 14,2017 IN NEWS

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Joseph Magufuli amerejesha ekari 129 kwa Wananchi wa kata ya Iyumbu- Jimbo la Dodoma Mjini katika eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya makaburi ya Viongozi wa Kitaifa.

Mh Magufuli amefanya maamuzi hayo jana baada ya kupokea maombi ya Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde wakati wa ufunguzi wa nyumba 300 za Shirika la Nyumba Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu,ambapo Mbunge Mavunde alimuomba Mh Rais kulirejesha kwa wananchi eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya makaburi ya Viongozi wa Kitaifa kwakuwa ni zaidi ya miaka 7 imepita bila wananchi kulipwa fidia yoyote na kushindwa kuyatumia maeneo hayo kwa shughuli za kilimo na ufugaji kama walivyokuwa wanafanya awali.

Akijibu maombi ya Mh Mavunde,Rais Magufuli ameagiza ekari zote 129 zirejeshwe kwa wananchi kwa kuwa serikali haina mpango wa kulitumia eneo hilo kwa sasa.Uamuzi huo umepokelewa kwa shangwe na furaha kubwa sana na wananchi na kumpongeza sana Mh Rais kwa kuwajali wanyonge.

Aidha Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa kuwa na Mbunge mchapakazi na anayewajali wananchi wake na ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi yao.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Anthony Mavunde akizungumza katika hafla fupi ya ufunguzi wa nyumba 300 za Shirika la Nyumba Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu,Mjini Dodoma.






0 maoni:

Chapisha Maoni