Ijumaa, 1 Desemba 2017

BALOZI SEIF ALI IDDI AWATAKA WAISLAM KUIMARISHA IMANI

posted by Esta Malibiche on DEC 1,2017 IN NEWS

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewataka Waislam nchini kote kuwa waadilifu kama alivyokuwa Mtume Muhammad (S.A.W).
Amesema ni vema wakatumia wakati huu wa Maulid kutathmini mienendo ya maisha yao kwa kujiuliza kama maisha wanayoishi  yanafanana na yale aliyoishi Mtume Muhammad.
Balozi Seif ameyasema hayo leo (Ijumaa, Desemba Mosi, 2017) alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza la Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) lililofanyika kitaifa wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi.
“Kuna vigezo vingi mja anaweza kuvitumia wakati anapojitathmini, ambavyo ni pamoja na tabia ya Bw Mtume ya uadilifu na  wake. Tujiulize kati yetu hapa ni wangapi waadilifu na waaminifu kama alivyokuwa Bw. Mtume.”
Amesema kupungua kwa uaminifu na uadilifu ndiko kulikomfanya Rais Dkt. John Magufuli mara baada ya kuingia madarakani kuanzisha vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi, hivyo wanatakiwa kumuunga mkono.
 “Mtume (S.A.W) aliikemea sana rushwa na akasema kuwa amelaaniwa na Mwenyezi Mungu mwenye kutoa na kupokea rushwa na hata Yule mpiga debe. Pia tunaamini kuwa dini zote duniani zinapinga rushwa, hivyo tuiiepuke” 
Awali, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Bin Zubeiry alisema aliwaasa Watanzania wote waendelee kuidumisha na kuitunza amani kwa sababu hakuna maendeleo yoyote yatakayopatikana bila ya kuwepo kwa amani.
Alisema suala la kudumisha amani, kuheshimiana na kushirikiana miongoni mwa waislamu na wasiokuwa waislam limehimizwa sana katika dini ya kiislam na dini nyingine, hivyo wananchi hawana budi kuendeleza.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza Sheikh Mkuu kwa uongozi wake mzuri wa  Baraza la WaislamTanzani (BAKWATA) ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na dini zote bila Ubaguzi.
Alisema serikali itaendelea kufanya kazi na dini zote na kwamba Rais Dkt. Magufuli amezipa kipaumbele shughuli za dini zote ziendelee kufanyika nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika Baraza la Maulidi ya  Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika kwenye  uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Rungwa Desemba 1, 2017. Mgeni Rasmi katika Maulidi hayo alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Baraza la Maulidi ya  Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika kwenye  uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Rungwa Desemba 1, 2017. Mgeni Rasmi katika Maulidi hayo alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Mufti Mkuu wa Tanzania,  Sheikh Aboubakar Zubeiry akizungumza katika Baraza la Maulidi ya  Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika kwenye  uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Rungwa Desemba 1, 2017. 
Baadhi ya washiriki wa Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) wakimsikiliza Mgeni Rasmi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati alipohutubia   kwenye uwanja wa  Shule ya Msingi ya  Likangala wilayani   Ruangwa Desemba 1, 2017.

0 maoni:

Chapisha Maoni