Jumatatu, 27 Machi 2017

KIWANDA CHA SARUJI MOSHI CHAFUNGWA KWA UCHAFUZI WA MAZINGIRA

Posted by Esta Malibiche on MARCH 27,2017 IN NEWS

UCHA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Rombo Bi. Agness Hokororo mara baada ya kuwasili wilayani hapo kwa ziara ya kikazi.
UCHA 1
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba alipotembelea kiwanda cha saruji cha Moshi. Kiwanda hicho kimefungiwa baada ya kutotekeleza maagizo waliyopewa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Katikati ni Mwakilishi wa Kiwanda hicho Bi. Sophia na kushoto ni Dkt. Menan Jangu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Kanda ya Kaskazini.
UCHA 2
Mtambo wa kudhibiti vumbi katika kiwanda cha saruji cha Moshi ambao haufanyi kazi ipasavyo, kumekua na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya uchavuzi wa hewa ufanywao na kiwanda hicho. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Kanda ya Kaskazini ilitoa maelekezo ambayo hayakutekelezwa kikamilifu,  hivyo kiwanda hicho kimefungwa hii leo.
……………
Na Lulu Mussa,Moshi
Ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba hii leo ametembelea Mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Rombo. Akiwa Wilayani hapo Waziri Makamba ametembelea Kiwanda cha Saruji cha Moshi kufuatia malalamiko ya wananchi juu ya uchafuzi wa hewa itokanayo na vumbi katika shughuli za uzalishaji.
Akitoa maelezo wa awali, Mkuu wa Wilaya ya Rombo Bi. Agness Hokororo amesema kuwa Kiwanda hicho kimeendesha shughuli za uzalishaji wa sementi kwa kutofuata sheria ya mazingira ya mwaka 2004 ikiwa ni pamoja na kutokuwa na mfumo mzuri wa kudhibiti uchafuzi wa vumbi kiwandani hapo.
kwa upande mwingine Dkt. Menan Jangu Mratibu wa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Kanda ya Kaskazini amesema kuwa Ofisi yake awali ilitembelea kiwanda hicho na kutoa muongozo na taratibu zinazotokiwa kufuatwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
“Tuliwaelekeza kufanya yafuatayo, kujenga fensi kuzunguka eneo lote la kiwanda, kujenga “pevements” na kuweka mashine maalumu ya kuzuia vumbi kusambaa kwa wingi angani, vitu ambavyo havijafanyiwa kazi.” Alisisitiza Dkt. Jangu
Mwakilishi wa Kiwanda hicho raia wa China aliyefahamika kwa jina moja tu Bi. Sophia, amesema kuwa suala la kuzungusha uzio eneo lote litatekelezwa pindi hati miliki ya ardhi ya eneo hilo itakapopatikana.
Waziri Makamba aliagiza NEMC kukifunga kiwanda hicho mpaka mapendekezo yaliyotolewa na Baraza yatakapokamilika. “Kiwanda hiki kisitishe shughuli za uzalishaji mpaka pale vigezo vya Sheria ya Mazingira vitakapokamili”
Katika hatua nyingine Waziri Makamba ametembelea Ziwa Chala na kuwataka wadau wa mazingira kuongeza jitihada katika kulihifadhi  kwa kuwa ni muhimu kwa ikolojia na historia yake. ” Kina cha ziwa hili kinashuka kwa kasi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na sisi kama Serikali tutahakikisha tunawekeza nguvu zetu katika kunusuru kina cha ziwa hili kisiendelee kushuka” Alisisitiza Makamba.
Waziri Makamba ameahidi kuzungumza na Serikali ya Kenya ili kuwa na mikakati ya pamoja ya kuhifadhi ziwa hilo kwa kukuwa lipo pande zote za nchi hizi. Ziwa Chala ni chanzo kikubwa cha utalii na limetokana na mlipuko wa Volcano likiwa halitoi wala kuingiza maji kutoka vyanzo mbalimbali.
Waziri Makamba amemaliza ziara yake Mkoani Kilimanjaro na hii leo amewasili Mkoani Arusha.

0 maoni:

Chapisha Maoni