Jumatatu, 20 Machi 2017

WAZIRI MHAGAMA ARIDHISHWA NA JITIHADA ZA KUREJESHA MIUNDOMBINU MKOANI KAGERA

Posted by Esta Malibiche on MARCH 20,2017 IN NEWS.

FV
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akinukuu hoja za wajumbe wa kikao cha Tathimini ya Utekelezaji wa Miradi ya Kukabili na Kurejesha hali kwa maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko Mkoani Kagera kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkoa Machi 18, 2017 kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Dkt.Hamisi Mwinyimvua.
FV1
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Tathimini ya Utekelezaji wa Miradi ya Kukabili na Kurejesha hali kwa maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa kujadili na kupokea taarifa hiyo mkoani Kagera.
FV 2
Mkuu wa Wilaya ya Kagera Mhe. Deodatus Kinawilo akichangia hoja wakati wa kikao cha Tathimini ya Utekelezaji ya Kukabili na Kurejesha hali baada ya athari za tetemeko mkoani Kagera.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU).
……………………….
Na. Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama ameupongeza uongozi wa mkoa wa Kagera kwa hatua iliyofikiwa katika kurejesha miundombinu mbalimbali iliyoathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba10 mwaka 2016 katika Mkoa wa Kagera linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa 5.9 katika vipimo vya Richter.

Mhe. Mhagama alionesha kuridhishwa kwake baada ya kufanya ziara  Mkoani hapo mapema wiki hii kwa lengo la kutathimini utekelezaji unaoendelea katika kurejesha miundombinu ili wananchi waendelee kutumia huduma hizo kama kawaida.
Katika ziara hiyo, Waziri Mhagama alitembelea Shule ya Sekondari Nyakato, Ihumo na Omumwani, Kituo cha Afya cha Kabyaile-Ishozi na Kituo cha Kulelea Wazee cha Kiilima na kubaini kuwa ujenzi wa Kituo kipya cha Afya cha Kabyaile-Ishozi ambacho kimefikia asilimi 80 ambapo kimetumia kiasi cha shilingi 381, 506, 079.00.
“Nikiri kwamba ukiacha baadhi ya mapungufu kwa watendaji wachache, wengi mmetupa ushirikiano mzuri kwa kulinganisha hali ilivyokuwa kwa kuangalia tukio lilivyotokea na hadi hatua za kukabili hatimaye kurejesha hali.”Alisema Waziri
Aliendelea kushukuru ushirikiano mzuri uliopo katika kutekeleza majukumu hatimaye kufikia lengo “Kama sio ushirikiano wa pamoja kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkoa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania huwenda tusingefika hapa hivyo tuna kila sababu ya kupongeza juhudi hizi kwa niaba ya Serikali hususani Ofisi ya Waziri Mkuu tumefarijika kwa ushirikiano wenu”
Pamoja na pongezi hizo, Waziri alimtaka Katibu Tawala wa Mkoa Kamishna Diwani Athuman kuendelea kuzingatia taratibu za manunuzi na kila eneo linalofanyiwa kazi kufuata taratibu, kanunuzi zilizopo kwani kwa atakaye kiuka sheria na taratibu hakutakuwa na msamaha.”Hakutakuwa na msamaha kwa yeyote atakayefanya uzembe lazima sheria zichukue mkondo wake hakuna kuoneana aibu” Alisisitiza waziri.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mhe. Deogratius Kinawilo alipongeza kwa kukiri kuwa kazi inayoendelea ya kurejesha hali imefanyika kwa umakini mkubwa. “Tumefanya kazi kwa umakini mkubwa na kila mmoja alikaa kwenye nafasi yake hivyo niendelee kuwaomba watendaji wote kufuata sheria na kutekeleza yote yanayotupasa ili kuokoa mazingira ya wanakagera kwa ujumla”
Waziri mhagama alieleza pia pamoja na jitihada zote ifike mahali kile kilichokusudiwa kitimie na miradi yote ifikapo mwezi Mei mwaka huu imekamilika” Tuendelee kutekeleza majukumu yetu katika zoezi la kurejesha hali ili ifikapo mwezi Mei angalau asilimia 80 iwe imekamiliza” Alisema waziri
Ziara hiyo ilikuwa ni moja ya utekelezaji wa maagizo ya Mhe.Rais John Pombe Magufuli aliyoyatoa wakati wa ziara yake Januari mwaka huu na kuiagiza  Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya tathimini za shughuli zote wakati wa kukabili na urejesha hali baada ya kutokea kwa Tetemeko hilo.

0 maoni:

Chapisha Maoni