Jumatatu, 6 Machi 2017

JPM abariki TANESCO kuwakatia umeme wadaiwa sugu

Posted by Esta Malibiche on MARCH 6,2017 IN NEWS
Rais John Pombe Magufuli, amelipongeza Shirika la Umeme Nchini, (TANESCO) kutokana na kasi yake ya kusambaza umeme nchini hususan vijijini.
 Rais aliyasema hayo Machi 5, 2017 wakati akizindua Mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme wa 132kv mkoani Mtwara.
Mradi huo utakamilika Mei 30, 2017 na kitahudumia mikoa ya Mtwara na Lindi na hivyo kutatua kero ya upatikanaji umeme kwenye mikoa hiyo ambayo shughuli za kiuchumi zimeongezeka sana. Awali kituo hicho kwa sasa kina uwezo wa 33kv.
“TANESCO mmenifurahisha sana kwa kutekeleza vema ilani ya uchaguzi ya CCM, kwa kuhakikisha wanachi kote nchini wakiwemo wa vijijini wanapatiwa umeme,” alisema. 
 Rais pia alisema, anatambua changamoto zinazolikabili shirika hilo hususan madeni ya bili za umeme kwenye taasisi za serikali.
“Ninaagiza, wale wote wanaodaiwa bili za umeme na TANESCO, walipe madeni yao haraka, vinginevyo muwakatie umeme,” alisema Rais.
“Hata Ikulu kama inadaiwa we kata, najua pia kuna deni la shilingi Bilioni 162 Kule Zanzibar, nako kama hawatalipa kateni umeme. tunataka TANESCO iharakishe kusambaza umeme kwa wananchi sasa wasipolipwa madeni watawezaje kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi?,” aliuliza Rais Magufuli.
Aidha kutokana na kufurahishwa na kasi ya TANESCO kusambaza umeme kwenye maeneo Mengi ya nchi, amesema ofisi yake iko tayari kusaidia fedha pale itakapoonekana kuna mkwamo wa kifedha katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya umeme.
NA K-VIS BLOG
 Rais Magufuli(wapili kushoto), Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo(watatu kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt.Alexander Kiaruzi, na Mwenyekiti wa CCC mkoa wa Mtwara, wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo hicho.
Rais akiandika kitu, wakati akiteta na Profesa, Muhongo wakati wa uzinduzi huo.
 Rais Magufuli akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa TANESCO baada ya kupiganao picha.
Share:

0 maoni:

Chapisha Maoni