Posted by Esta Malibiche on MARCH 27,2017 IN NEWS
MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza
amewataka watoa huduma katika sekta ya ukarimu na utalii kanda ya kusini kuboresha
huduma zao ili kukidhi haja soko la utalii katika ukanda huu.
Mafunzo hayo yanayotolewa na wizara
ya Maliasili na utalii kwa kushirikiana na Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo
Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), yanafanyika kwa muda wa siku
tatu Iringa.
Aliyasema hayo jana kwenye mafunzo
ya siku tatu kwa watoa huduma wa sekta ya ukarimu na utalii,na kuhudhuriwa na watoa huduma zaidi ya 80 wanaofanya biashara
inayohudumia watalii mkoani Iringa.
Masenza alisema kuwa ili kuongeza
idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za taifa za kusini watoa huduma kwa
kushirikiana na sekta binafsi hawanabudi kuinua viwango vya utowaji wa huduma.
Alisema kuwa serikali ipo katika
machakato wa kuboresha miundombinu za barabara na viwanja vya ndege ili kurahisha
watalii kufika katika hifadhi pamoja na vivutio vilivyopo katka ukanda wa
kusini.
‘’Takwimu za mwaka 2015 zinaonesha
kuwa watalii wengi zaidi walitembelea mbuga za kanda za kaskazini kuliko kanda
ya kusini, kwa hiyo mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuboresha utoaji wa huduma
katika kanda ya kusini.Hivyo basi Wizara ya Maliasili na Utalii ipo katika mchakato wa
kutunga kanuni zitakazowazuia wafanyakazi wa hoteli wasio na vyeti
vinavyotambulika na serikali kutoa huduma katika sekta ya utalii’’Alisema
Masenza
Alisema kuwa kanuni hiyo ambayo
msingi wake unalenga kuendeleza na kuboresha huduma katika ya sekta hiyo,
utahusisha pia kuvibana vyuo vya hoteli na utalii ili vitoe mafunzo yanayokidhi
viwango kwa manufaa ya Taifa.
“Baada ya kutungwa na kuanza
kutumika kwa kanuni hizo, waajiri katika sekta hiyo watalazimika kuwaajiri
wafanyakazi wenye sifa ambao wamesajiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii,”
alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utalii, alisema Masenza.
Kwa upande wake Mratibu wa SPANEST,
Godwell Ole Meing’ataki alisema changamoto hizo zimesababisha huduma duni
katika maeneo ya mapokezi, chakula, vinywaji na malazi, na hivyo kuleta
malalamiko makubwa sana kwa wageni.
Meing’ataki alisema SPANEST inamatarajio
makubwa mara mafunzo yatakapomalizika washiriki wataweza kutambua wajibu wao
ili wageni waingiapo waweze kuwahudumiwa vizuri.
“Sekta ya utalii ina changamoto
nyingi, lakini eneo hili la huduma ni muhimu kwasababu linaweza kusaidia
kumrudisha mgeni tena na tena na kumfanya awe balozi kwa watu wengine,” alisema
Meing’ataki .
Aliongeza kuwa katika sekta ya
utalii haitoshi kuwa na hoteli kubwa tu kama
itakuwa haina huduma bora kwa wageni wake.
Awali,Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa
Iringa, Fikira Kissimba alisema licha ya ukanda wa nyanda za juu kusini kuwa na
vivutio vingi vya utalii, idadi ya watalii wanaovitembelea ni ndogo na moja ya
sababu yake ni uduni wa huduma katika sekta hiyo ya utalii.
Kissimba aliishukuru wizara ya
maliasili na utalii na SPANEST kwa kutoa mafunzo hayo, Kissimba alisema
yatakuwa chachu katika kukuza na kuendeleza utalii kusini mwa Tanzania kwa
kutoa huduma bora kwa watalii.
Aliwataka wahudumu katika sekta hiyo
waache tabia ya uvivu, kufanyakazi kwa mazoea na wawe wepesi kujifunza ili
kuboresha huduma zao.
0 maoni:
Chapisha Maoni