Jumatano, 15 Novemba 2017

Mikoa ya Dar, Pwani na Morogoro yashauriwa kufuata sheria za uhifadhi wa maliasili

Posted by Esta Malibiche on NOV.15.2017 IN NEWS
Inline image 1
Na Tulizo Kilaga


WANANCHI katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Dar es Salaam inayopatikana kanda ya mashariki wametakiwa kuzingatia umuhimu wa hifadhi za misitu nchini kwa kuhakikisha kila mwananchi anazingatia maagizo ya Serikali pamoja na kufuata sheria za nchi zinazohusiana na uhifadhi wa maliasili.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo, mkoani Morogoro wakati akifungua mkutano wa siku moja wa kanda ya mashariki kuhusu utekelezaji wa randama ya makubaliano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) ulioandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na kufanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), tarehe 9 Novemba, 2017.

Mkuu wa Mkoa huyo wa Pwani ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo alisema randama hiyo iliyosainiwa na pande hizo mbili imelenga kuimarisha usimamizi wa misitu nchini na utawala bora, kufanya Uperembaji wa Miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Misitu Tanzania na Kuboresha ukusanyaji, ugawaji, utumiaji na kufuatilia matumizi ya asilimia tano ya tozo ya upandaji miti.

Injinia Ndikilo alisema, inasikitisha kuona dhamana ya kudhibiti uharibifu mkubwa wa misitu unaofikia kiasi cha hekta 372,000 kwa mwaka ambacho ni sawa na asilimia 1.1 ya eneo lote lenye misitu inayokadiriwa kuwa hekta milioni 48 na sawa na kufyeka zaidi ya hekta 1,000 kwa siku wanaachiwa TFS.

Alisema tafiti zinaonyesha kuwa utegemezi mkubwa wa misitu kwa ajili ya nishati (mkaa na kuni), hususani katika mkoa wa Dar es salaam unachangia nusu ya uharibifu wa misitu nchini.

Mkuu wa Mkoa huyo aliongeza kuwa zaidi ya asilimia sabini ya mkaa unaozalishwa mikoani huingia Dar es Salaam kwa njia zisizo halali kama vile magari yaliyofunikwa, baiskeli na pikipiki, na endapo hatua madhubuti za kudhibiti uharibifu huo hazitachuliwa kwa haraka nchi itakuwa jangwa siku za karibuni.

Injinia Ndikilo alisema juhudi za pamoja zinatakiwa katika kuilinda na kuhifadhi misitu yetu, na kuwataka viongozi waliofika katika mkutano huo kuondoka wakiwa wamepikwa hasa kwa kuwa wamejadili mambo mbalimbali kuhusu usimamizi wa misitu na majukumu ya kila mdau katika kuhifadhi na kuilinda.

Aidha, aliwasihi viongozi waliohudhulia kuhakikisha mikakati na maazimio waliyojiwekea hayabaki katika makabati ya ofisi zao bali yawe kwenye utekelezaji wa kazi zao za kila siku na kuhakikisha kila mwananchi anazingatia maagizo ya Serikali pamoja na kufuata sheria za nchi zinazohusiana na uhifadhi wa maliasili.

“Naagiza, wale wote wanaofanya biashara ya mkaa kuzingatia sheria na taratibu ikiwamo uzito wa gunia la mkaa uliowekwa (kilo 50). Ni marufuku mazao ya misitu kusafirishwa na vyombo visivyoruhusiwa kisheria, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaesafirisha, kununua au kuuza mazao yaliyovunwa kinyume na sheria,” alisema injinia Ndikilo.

Mkurugenzi wa mipango na matumizi endelevu ya misitu na nyuki nchini, Mohamed Kilongo alisema TFS imekuwa ikitoa elimu inayohusu usafirishaji wa mazao ya misitu hususan mkaa baada ya kubaini mkaa kuwa ndio kichocheo kikubwa cha uharibifu wa mazingira kutokana na kuvunwa kinyume na taratibu na kusafirishwa kwa kutumia pikipiki na baiskeli jambo ambalo ni kinyume na sheria.

“Usafirishaji wa mazao ya misitu kwa baiskeli na pikipiki unakiuka Mwongozo wa Uvunaji Endelevu wa Mazao ya Misitu, 2015 unaoeleza kuwa vyombo vya usafiri vinavyoruhusiwa kusafirisha mazao ya misitu ni vile vyenye magurudumu manne,” alisema Kilongo.

Aidha, alisema mwongozo huo ulizingatia pia sheria nyingine za nchi zikiwemo Sheria za Usalama wa Barabarani na Sumatra, lakini pia kubana mianya ya wizi na ukwepaji mkono wa sheria za usimamizi wa maliasili nchini.

“Kwa upande wa Sumatra kupitia Kanuni ya Leseni za Usafirishaji ya Mwaka 2010, inatambua pikipiki kama chombo cha kusafirisha abiria na si vinginevyo na Sheria ya Usalama Barabarani Sura Namba 168 iliyorejewa mwaka 2002 inatambua pikipiki na baiskeli kama chombo cha usafirishaji kwa ajili ya abiria na si mizigo,” alisisitiza.

Aidha, alisema kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika Novemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu, katika barabara kuu za Bagamoyo, Kisarawe, Morogoro na Kilwa zinazoingia jijini Dar es Salaam, jumla ya pikipiki 582 zimebainika kubeba mazao ya misitu kinyume cha sheria kila siku.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bi. Sophia Mjema alisema inasikitisha kuona kuwa sheria zipo na wanaosimamia hawatekelezi wajibu wao hali inayopelekea misitu kuendelea kuisha.

“Inawezekanaje vyombo vinavyosafirisha mazao ya msitu kinyume na sheria, hususan baiskeli na pikipiki vinapita mbele ya askari wa usalama barabarani na hachukuliwi hatua? Inawezekanaje hawa wanapita na magunia yenye uzito zaidi ya unaostahili? Inawezekana vipi Halmashauri inaukatia ushuru mzigo huo? Inawezekanaje anapita kwenye vizuizi vyenye watu wa usalama baada ya giza kuingia ili hali hairuhusiwi? Kila mtu na atimize wajibu wake misitu yetu itapona,” alisema Bi. Mjema.

Baadhi ya wananchi wanaipongeza Serikali kwa kuwabana wenye baiskeli na pikipiki kutojihusisha na biashara hiyo, hivyo kutumika kama chanzo au kichocheo cha uvunaji holela na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu kutoka misitu ya hifadhi, mapori ya akiba na hata hifadhi za Taifa.

 “Naipongeza Serikali sasa kwa kuona umuhimu wa kukumbushana kila mmoja atimize wajibu wake ipasavyo katika kuimarisha usimamizi wa misitu nchini na hii itaokoa nchi yetu kuepukana na majanga ya mafuliko, upepo mkali na hata biashara yetu ya utalii tutakuwa na uhakika nayo kwa kuwa wanyamapori watakuwa salama kwenye makazi yao,” anasema Kabalo Kaseka, mkazi wa Temeke Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Jumla ya wajumbe 80 kutoka Halmashauri za wilaya 19, Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na Washauri wa Maliasili wa Mikoa ya Kanda ya mashariki, Maafisa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dodoma na Menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wamehudhuria mkutano huu.


 

0 maoni:

Chapisha Maoni