Posted by Esta Malibiche on MARCH 27,2017 IN NEWS
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akisalimiana na Mkuu wa
Wilaya ya Rombo Bi. Agness Hokororo mara baada ya kuwasili wilayani hapo
kwa ziara ya kikazi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba alipotembelea kiwanda cha
saruji cha Moshi. Kiwanda hicho kimefungiwa baada ya kutotekeleza
maagizo waliyopewa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC). Katikati ni Mwakilishi wa Kiwanda hicho Bi. Sophia na
kushoto ni Dkt. Menan Jangu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira Kanda ya Kaskazini.
Mtambo wa kudhibiti vumbi katika
kiwanda cha saruji cha Moshi ambao haufanyi kazi ipasavyo, kumekua na
malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya uchavuzi wa hewa ufanywao na
kiwanda hicho. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC
Kanda ya Kaskazini ilitoa maelekezo ambayo hayakutekelezwa kikamilifu,
hivyo kiwanda hicho kimefungwa hii leo.
……………
Na Lulu Mussa,Moshi
Ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba hii leo
ametembelea Mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Rombo. Akiwa Wilayani
hapo Waziri Makamba ametembelea Kiwanda cha Saruji cha Moshi kufuatia
malalamiko ya wananchi juu ya uchafuzi wa hewa itokanayo na vumbi katika
shughuli za uzalishaji.
Akitoa maelezo wa awali, Mkuu wa
Wilaya ya Rombo Bi. Agness Hokororo amesema kuwa Kiwanda hicho
kimeendesha shughuli za uzalishaji wa sementi kwa kutofuata sheria ya
mazingira ya mwaka 2004 ikiwa ni pamoja na kutokuwa na mfumo mzuri wa
kudhibiti uchafuzi wa vumbi kiwandani hapo.
kwa upande mwingine Dkt. Menan
Jangu Mratibu wa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira Kanda ya Kaskazini amesema kuwa Ofisi yake awali
ilitembelea kiwanda hicho na kutoa muongozo na taratibu zinazotokiwa
kufuatwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
“Tuliwaelekeza kufanya yafuatayo,
kujenga fensi kuzunguka eneo lote la kiwanda, kujenga “pevements” na
kuweka mashine maalumu ya kuzuia vumbi kusambaa kwa wingi angani, vitu
ambavyo havijafanyiwa kazi.” Alisisitiza Dkt. Jangu
Mwakilishi wa Kiwanda hicho raia
wa China aliyefahamika kwa jina moja tu Bi. Sophia, amesema kuwa suala
la kuzungusha uzio eneo lote litatekelezwa pindi hati miliki ya ardhi ya
eneo hilo itakapopatikana.
Waziri Makamba aliagiza NEMC
kukifunga kiwanda hicho mpaka mapendekezo yaliyotolewa na Baraza
yatakapokamilika. “Kiwanda hiki kisitishe shughuli za uzalishaji mpaka
pale vigezo vya Sheria ya Mazingira vitakapokamili”
Katika hatua nyingine Waziri
Makamba ametembelea Ziwa Chala na kuwataka wadau wa mazingira kuongeza
jitihada katika kulihifadhi kwa kuwa ni muhimu kwa ikolojia na historia
yake. ” Kina cha ziwa hili kinashuka kwa kasi kutokana na athari za
mabadiliko ya tabianchi na sisi kama Serikali tutahakikisha tunawekeza
nguvu zetu katika kunusuru kina cha ziwa hili kisiendelee kushuka”
Alisisitiza Makamba.
Waziri Makamba ameahidi kuzungumza
na Serikali ya Kenya ili kuwa na mikakati ya pamoja ya kuhifadhi ziwa
hilo kwa kukuwa lipo pande zote za nchi hizi. Ziwa Chala ni chanzo
kikubwa cha utalii na limetokana na mlipuko wa Volcano likiwa halitoi
wala kuingiza maji kutoka vyanzo mbalimbali.
Waziri Makamba amemaliza ziara yake Mkoani Kilimanjaro na hii leo amewasili Mkoani Arusha.