Jumanne, 14 Februari 2017

Wananchi Simanjiro Wapongeza Mradi Wa Rafiki Power

Posted by Esta Malibiche on FEB 14,2017 IN NEWS

SIMA
Meneja Mkuu wa kampuni ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua ya  Rafiki Power, Joanis Holzigel (kushoto) akibadilishana mawazo na Mtaalam wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Emillian Nyanda (kulia)  katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizarani katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya umeme.
SIMA 1
Mmiliki wa kioski kilichonufaika na huduma ya umeme jua kupitia kampuni ya  Rafiki Power, Thadeo Bura (kushoto) akielezea manufaa ya mradi wake katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya umeme.
 SIMA 2
Moja ya kioski kilichonufaika na huduma ya umeme jua kupitia kampuni ya  Rafiki Power kilichopo katika kijiji cha Komolo wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
SIMA 3
Mmiliki wa mghahawa wa chakula ambaye ni mmoja wa wanufaika wa huduma ya umeme jua kupitia kampuni ya  Rafiki Power akionesha friji inayotumia nishati hiyo katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya umeme.
SIMA 4
Mmiliki wa kioski kilichonufaika na huduma ya umeme jua kupitia kampuni ya  Rafiki Power, Thadeo Bura akielezea matumizi ya  compressor inayotumia nishati ya jua kwa matumizi mbalimbali, katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya umeme.
……………….
  • Kampuni yajipanga kupatia kaya 20,000 umeme wa uhakika mwaka 2022
Na Greyson Mwase, Manyara
Februari 14, 2017
Wananchi katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamepongeza kampuni ya kuzalisha umeme  kwa kutumia  nishati ya jua ya  Rafiki Power iliyopo chini ya kampuni tanzu ya  E.ON ya Ujerumani, kwa kuwapatia huduma ya umeme iliyopelekea kukua kwa kasi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Waliyasema hayo leo katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika miradi ya umeme mkoani Manyara yenye lengo la kuangalia utekelezaji wa miradi ya umeme,  changamoto zake na kutoa ushauri wa kitaalam.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake katika kijiji cha Komolo kilichopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Thadeo  Bura ambaye ni mmiliki wa duka la vifaa vidogo vya umeme jua na bidhaa nyingine, alisema kabla ya kampuni ya Rafiki Power kuwekeza katika kijiji hicho maisha yalikuwa ni magumu kwa kuwa hakukua na nishati ya kuwawezesha kuanzisha miradi midogo midogo.
Alisema mara baada ya kupata umeme kupitia kampuni ya Rafiki Power, ameweza kuanzisha duka kwa ajili ya vifaa vidogo vya umeme jua, bidhaa nyingine na kutoa huduma nyingine kwa wanakijiji wenzake.
Alisema huduma ya umeme imewekwa kwenye baadhi ya shule na hospitali hivyo kuboresha huduma za jamii.
Naye Joseph Hango ambaye ni mmiliki wa saluni ya kunyoa nywele aliongeza kuwa uwepo wa nishati ya umeme kupitia kampuni ya Rafiki Power umepelekea kuongezeka kwa kipato kutokana na idadi ya wateja kuongezeka.
Aliiomba kampuni hiyo kuendelea na juhudi za kusambaza umeme katika maeneo mengi ambayo hayajafikiwa na huduma ya umeme ili kukuza uchumi wa wilaya na mkoa kwa ujumla.
Wakati huohuo, akizungumza katika ziara hiyo Meneja Mkuu wa Kampuni ya  Rafiki Power, Joanis Holzigel alisema kuwa kampuni yake inatarajia kuongeza uzalishaji wa umeme ambapo kaya 20,000 nchi nzima zinatarajiwa kunufaika na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2022.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa nishati ya umeme katika uchumi wa viwanda utakaopelekea nchi ya Tanzania kuwa  kwenye orodha ya nchi za kipato cha  kati ifikapo mwaka 2025, kampuni yake imeweka mipango ya muda mfupi na muda mrefu ambapo inatarajia kufikia wateja 20,000 ifikapo mwaka 2022.
Akitaja miradi inayotekelezwa na kampuni yake, Meneja Holzigel alisema katika mkoa wa Arusha kampuni yake ina miradi minne katika  maeneo ya Digodigo,  Soitsambu, Ololosokowani, na Malambo yaliyopo wilayani Ngorongoro na miradi mingine miwili iliyopo katika maeneo ya Itaswi na  Kwamtoro wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.
Aliongeza kuwa, mradi mwingine mmoja unaotekelezwa na kampuni hiyo ni  wa Komolo/Temeke, uliopo Simanjiro mkoani Manyara.

0 maoni:

Chapisha Maoni