Jumatatu, 6 Februari 2017

MZUZURI AWATAKA VIJANA KUTUMIA FURSA ZA KILIMO ZILIZOPO ILI KUJIINUA KIUCHUMI.

Posted by Esta Malibiche on FEB 6,2017 IN NEWS

Mbunge wa viti maalum kundi la vijana Mariam Ditopile Mzuzuri akiwa na vijana wa CCM katika shamba la zabibu lililopo Chinangali  wilayani Chamwino  mkoani Dodoma

 Wabunge wa viti maalum Mariam Ditopile Mzuzuri na Maria Kangoye wakiwa na vijana wa CCM akiwemo msanii Jokate Mwegelo wakipewa elimu ya namna ya kuotesha zabibu, changamoto zake na faida ya zao hilo.
 .Mbunge wa Viti maalum Kundi la vijana Mariam Ditopile Mzuzuri akizungumza na vijana wa CCM aliombatana nao kutembelea mashamba ya zabibu wilayani Chamwino mkoani Dodoma akieleza dhamira ya kuwapeleka katika shamba hilo


                        Mbunge wa Viti maalum kundi la vijana, Mariam Ditopile Mzuzuri akiwa na vijana wa CCM wakielekea lililopo shamba la Zabibu.

                .....................................................................................................................



MBUNGE wa viti maalum Mariam Ditopile Mzuzuri amewasihi vijana kujishughulisha na shughuli za kilimo hususan kilimo cha zabibu ili kujiinua kiuchumi na kuondokana na tatizo la ajira.

Hatua hiyo ni  kuunga mkono na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Rais Dk.John Magufuli ya hapa kazi tu na kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Mariam alitoa rai hiyo mjini hapa  wakati alipofanya ziara ya kutembelea Shamba la Zabibu la  Chinangali II, akiambatana na vijana wa Chama cha Mapinduzi kwa lengo la kujifunza namna ya uzalishaji, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM.

Alisema imefika wakati warudi na kuitekeleza kauli ya kama unataka mali utaipata shambani, ambayo itafanikiwa kwa watanzania kuwekeza kwenye shughuli za kilimo.

" kimsingi Zabibu ya Dodoma licha ya kutumika kutengeneza mvinyo ambao unasafirishwa ndani na nje ya nchi lakini bado haijatangazwa kiasi cha kutosha na kusababisha soko lake kuwa chini,"alisema Mariam.

Alisema imefika wakati vijana wa CCM kutumia fursa hiyo ikiwa ni pamoja na kuitangaza Zabibu ya Dodoma, na hasa ukizingatia kipindi hiki ambacho nchi inakwenda kuwekeza katika viwanda.

“Mimi kijana mwenzenu nawasihi mtumie vyema fursa hii ili muweze kujikwamua kiichumi, nimetumia nafasi hii kuwaleta ili mje kujifunza namna kilimo cha Zabibu kinavyotekelezwa ili nanyi muweze kuiga mfano huo kwa vitendo,”alisema.

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Maria Kangoye aliyeambatana na Mariam katika ziara hiyo, aliisihi  serikali yake sikivu ya CCM kuhakikisha inawawezesha vijana kikamilifu kupitia ile asilimia 5, ambayo ipo kisheria na imekuwa ikitengwa wakati wote.

Pia aliwasihi vijana wa CCM, kuacha kubweteka na badala yake wafanye kazi na kujitokeza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo.

Kwa upande wake Jokate Mwogelo ambaye pia aliambatana na mbunge Mariam katika ziara hiyo aliwataka vijana kutotumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kwa kuzungumza mambo yasiyofaa.

"Sisi vijana wa CCM tubadilike, tutumie mitandao hii kujiinua kiuchumi, tuelezane na kupashana habari za fursa zilizopo na hapo tutafanikiwa, alisema Jokate.

Shamba hilo la Zabibu la Chinangali II, hadi kufikia Julai 2016 lilikuwa na jumla ya ekari 295 ambazo zimeendelezwa kwa ruzuku kutoka serikali kuu na halmashauri ya wilaya ya Chamwino na mkopo wa Benki ya CRDB wa jumla ya Sh.bilioni 1.5.


Pia shamba  hilo lenye ukubwa wa ekari 1,250 lilianzishwa mwaka 2008 na  likikusudiwa kutoa mchango mkubwa wa kupunguza umasikini kwa vijana, wanawake na kutoa ajira kwa jamii ya vijiji sita vinavyozunguka eneo la mradi.

0 maoni:

Chapisha Maoni