Posted by Esta Malibiche on JAN 31,2018 IN NEWS
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Mji
wa Mafinga limeagiza mamlaka zinazohusika kufanya uchunguzi wa matumizi hewa ya
fedha zilizotolewa kwa ajili ujenzi wa nyumba
ya mwalimu katika shule ya msingi Ihumo na atakayebainika achukuliwe hatua za
kisheria ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kazi.
Jumla ya Sh 2,650,000 zikiwemo Sh Milioni
2 zilizotolewa na halmashauri hiyo na Sh 650,000 zilizotoka kwenye Mfuko wa
Jimbo la Mafinga Mjini, ziliingizwa katika akaunti ya shule hiyo mapema mwaka
jana na matumizi yake yakafanywa kati ya mwezi Mei na Julai.
Akisoma taarifa ya mkaguzi wa ndani wa
halmashauri hiyo kwenye baraza hilo juzi, diwani wa kata ya Saohill, Denis
Kutemile alisema katika kipindi hicho kulikuwepo na awamu mbili ya manunuzi ya
sementi na vifaa vingine vya ujenzi kwa ajili ya nyumba hiyo.
Kutumile alisema kwa kupitia risiti ya
kwanza ya manunuzi hewa inaonesha jumla ya Sh 840,000 zilitumika kununua mifuko
70 ya sementi lakini katika hali ya kushangaza ilikutwa mifuko 13 tu katika
stoo ya shule hiyo.
“Baada ya manunuzi hayo yalifanywa
manunuzi mengine hewa ya vifaa vya ujenzi ambayo kwa kupitia risiti yake
yanaonesha jumla ya Sh 650,000 zilitumika,” alisema na kutoa hoja ya kuliomba
baraza hilo liamuru uchunguzi ufanyike na muhusika wa matumizi hayo hewa
asimamishwe kazi.
Akipigilia msumari hoja hiyo, mwenyekiti
wa halmashauri hiyo, Charles Makoga alisema matumizi hayo hewa yamesababisha
pia ujenzi wa nyumba hiyo usimame na akaziomba mamlaka zinazohusika zifanye
uchunguzi huo haraka kwani umeathiri maendeleo ya sekta hiyo katika shule hiyo.
Wakati huo huo, baraza hilo limeagiza
hatua kali zichukuliwe kwa watoa huduma wa zahanati ya Bumilahinga
wanaotuhumiwa kutowasilisha kunakohusika zaidi ya Sh Milioni 2 zilizochangwa na
wananchi wa kijiji hicho mwaka jana waliochangia huduma za matibabu kwa hiari
kwa njia ya kadi (Tiba kwa Kadi-TIKA).
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo alisema
hiyo ni mara ya pili kwa watoa huduma wa zahanati hiyo kufanya hivyo, mara ya
kwanza ikiwa ni mwaka 2016 na hivyo kusababisha walengwa kukosa huduma
walizotarajia kuzipata katika kituo hicho.
“Tika ni shida katika zahanati ya
Bumilahinga, watu wanachanga fedha lakini zinakaa mifukoni mwa watu na
kusababisha wananchi wakose huduma za afya. Tunadhani wahusika wanatumia fedha
hizo kufanyia mambo yao na kuzirudisha baada ya ukaguzi kufanyika. Baraza
linataka wahusika wachukuliwe hatu kali,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,
Rajabu Gogwa aliahidi kufuatilia utekelezaji wa maagizo hayo na lingine
linaloitaka halmashauri hiyo kujitangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Katika hatua nyingine halmashauri hiyo
imeahidi kushirikiana na wadau wake wote kuendeleza mapambano dhidi ya
maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) yanayoendelea kuathiri nguvu kazi yao.
Makoga alisema halmashauri yake ni moja kati ya halmashauri za mkoa wa Iringa yenye kasi kubwa ya maambukizi hayo jambo linalotishia ustawi wa watu na maendeleo ya halmashauri hiyo.
0 maoni:
Chapisha Maoni