Jumapili, 4 Machi 2018

MIRADI YA KUJITOLEA YA UJENZI WA ZAHANATI YASHIKA KASI MUSOMA VIJIJINI

Posted by Esta Malibiche on March 4,2018 IN NEWS

  Hatua ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mkirira kilichopo jimbo la Musoma  Vijijini .

Na Fedson Masawa, Msaidizi wa Mbunge.

Miradi na Harakati za ujenzi wa zahanati zinazidi kushika kasi ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini na kufufua matumaini makubwa kwa wananchi wa Jimbo hilo ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwenye vijiji vyao.

Hayo yamebainika baada ya Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini kutembelea eneo la ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mkirira, Kata ya Nyegina na kushuhudia kazi ya ujenzi wa Zahanati inayoendelea katika eneo hilo.

Akizungumza na Msaidizi wa Mbunge, Mtendaji wa Kijiji cha Mkirira, Iddy Rukonge alisema, wananchi wazawa na wapenda maendeleo wa Kijiji hicho waishio nje ya Jimbo la Musoma Vijijini wapo tayari kuungana na wananchi na Mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo katika ujenzi wa Zahanati ya Kijiji chao ili kuwarahisishia ndugu zao upatikanaji wa huduma ya afya karibu na maeneo wanayoishi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi na wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Mkirira walisema tayari wamefikia hatua ya msingi (jamvi) kwa kutumia michango yao ya hali na mali na kuthibitisha kuwa, umoja na mshikamano wa serikali na wananchi Kijijini hapo ni nyenzo pekee itakayowasaidia kukamilisha ujenzi wa Zahanati yao kwa wakati kwa kuzingatia uhitaji wa huduma hiyo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyegina Majira Mchele alisema, hatua waliyofikia wananchi wa Mkirira inaleta matumaini ukilinganisha na muda walioanza ujenzi huo na kuahidi kushirikiana na wananchi na wapenda maendeleo wa Kijiji hicho pamoja na wafadhili kufanikisha ujenzi wa Zahanati hiyo mapema.

Naye Paschal Magati ambaye ni mwananchi mkazi wa Kijiji cha Mkirira alisema: "kwa kuwa Mbunge wetu wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ni Mbunge mpenda maendeleo, kwa kushirikiana na Serikali tutakuwa ni sehemu ya ratiba yake ili afike aone jitihada zetu wananchi na kuungana na sisi kufanikisha zoezi la upatikanaji wa huduma ya afya Kijijini Mkirira."

Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini kwa kushirikiana na Mbunge wao wamehamasika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya vijijini kwa kujenga zahanati katika vijiji mbalimbali, zoezi ambalo ukiachilia mbali elimu na kilimo, nalo limeonekana kuwa kipaumbele cha maendeleo Jimboni, ambapo zaidi ya Vijiji 10 vinaendesha Miradi ya ujenzi wa zahanati huku zahanati nne za Kigeraetuma, Chirorwe, Mwiringo na Mmahare zikiwa zimefikia katika hatua nzuri ya utekelezaji na zitaanza kutumiwa hivi karibuni. Jimbo lina Kituo cha Afya cha kisasa kwenye Kijiji cha Murangi (Makao Makuu ya Jimbo) ambao upasuaji (operation) unaweza kufanywa wa wagonjwa wawili kwa wakati mmoja. Elimu, Afya na Kilimo, na viwezeshaji kazi vyake (k.m. maji, umeme na barabara) vinatiliwa mkazo sana Jimboni.





0 maoni:

Chapisha Maoni