Jumamosi, 3 Machi 2018

PROF. MUHONGO ADHAMIRIA KUPUNGUZA UMASIKINI JIMBONI KWAKE

Posted by Esta Malibiche on March 3,2018 IN NEWS

Mbunge wa Musoma Vijijini Mkoani Mara kupitia Chama cha Mapinduzi CCM,Profesa,Sospeter Muhongo,akikabidhi mbegu za Ufuta na Alizeti kwa wananchi wake.

Mbunge wa Musoma Vijijini kupitia Chama cha Mapinduzi CCM,Profesa Sospeter Muhongo kwa kushirikiana na Wananchi wake wamedhamiria kutokomeza umasikini kupitia kilimo cha mazao mbalimbali ya biashara ikiwemo Pamba, Alizeti na Ufuta.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mbegu za Alizeti na Ufuta Machi 3, 2018, Mbunge huyo alisema ameungana na wananchi wake kuhakikisha wanaimarisha kilimo cha mazao ya biashara ili kuongeza mapato kupitia kilimo  na kuondokana na adui umasikini.

Profesa Muhongo alisema kuwa msimu huu ni watatu wa kilimo cha zao la Alizeti Jimboni humo ambapo wananchi wameweza kwa kiasi kikubwa kunufaika na zao hilo.

Alibainisha kuwa wawekezaji binafsi wamefunga mitambo ya kusindika  zao la Alizeti  katika Kijiji cha Kusenyi na  Saragana kwa ajili ya kukamua mafuta  na Mashudu.

Aliongeza kuwa matarajio ya baadaye katika siku zijazo ni kuweka mizinga ya nyuki kwenye mashamba ya alizeti ili wananchi waweze kulina Asali na kujikwamua kiuchumi.

Aidha akizungumzia mazao ya chakula, Profesa Muhongo alisema kuwa, tayari mbegu za Mihogo na Mtama ziligawiwa kwa wananchi jimboni humo ili waweze  kuondokana na adui njaa.

Wakati huo huo, Profesa Muhongo alikagua shamba la Pamba lililopo katika Kijijini cha Kinyang'erere, Kata ya Bugwema ili kujionea hatua iliyofikiwa.

Kwa Mujibu wa Mbunge huyo, jumla ya Vijiji 68 vilivyopo katika Kata 21 Jimboni humo vimenufaika na Mbegu za Alizeti na Ufuta.






0 maoni:

Chapisha Maoni