Posted by Esta Malibiche on March 29,2018 IN NEWS
Na Esta Malibiche
Mufindi
SHULE ya sekondari ya wasichana ya Regina Pacis inamilikiwa na kanisa katoliki parokia ya Kibaoni jimbo katoliki la Iringa tayari imeanza ujenzi wa vyumba nane vya madarasa ambapo mdau wa maendeleo mkoani Iringa,Josepht Mwagala amekabidhi mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya shilingi millioni 1.3 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Awali shule hiyo iliyopo katika kata ya Kibaoni wilayani humo, ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya miundombinu ya madarasa lakini kwa sasa yameanza kwa muundo wa ghorofa ambavyo vitawezesha watoto wa kike wa kidato cha tano kuanza masomo shuleni hapo mwaka huu 2018.
Akizungumza jana wakati wa kukabidhi msaada huo Mwagala alisema kuwa ametekeleza ahadi yake aliyotoa wakati wa mahafi ya kidato cha nne ya shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana na kujionea mradi mkubwa wa maendeleo wa ujenzi wa shule hiyo pamoja na changamoto zake na ndio maana ameamua kufanya hivyo.
“Nimeamua kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt.John Magufuli kwa kuboresha miundombinu na hii ni sehemu tu ya msaada wangu,nimevutiwa na miradi ya elimu inayotekelezwa katika kijiji hiki , niseme tu hiyo ni sehemu ya msaada lakini pale nitakapoona ninakitu cha kufanya hapa nitaendelea kuwasaidia kadri ya uwezo wangu.”alisema Mwagala
Pamoja na masaada huo pia ameahidi kuwa atahakikisha anajichanga kadri ya uwezo wake kuhakikisha anasaidia kutatua kero ya maji inayoikabili parokia na shule hiyo kwa sababu kwa kuwa msaada huo pia utawasaidia wananchi wa kijiji hicho na vijiji vya jirani.
Akipokea mifuko ya saruji hiyo mkuu wa shule hiyo ambae ni paroko wa parokia ya Kibaoni padre Cesco Muyinga alimshukuru Mwagala kwa kutoa msaada huo na kutoa wito kwa wadau wengine hususani wenye uwezo kujenga utamaduni wa kusaidia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo wanayotoka kama sehemu ya kurejesha fadhili kwa jamii waliowaacha katika maeneo hayo.
Padre Muyinga alisema msaada huo umefika wakati mwafaka kwa kuwa majengo ya shule hiyo yanatarajia kuanza kutumika wakati wowote kuanzia sasa.
" Kimsingi umetusaidia sana,kwani tangu uje kwenye mahafali yetu na kuona changamoto aliahidi kusaidia utatuzi wa tatizo la maji jambo ambalo unaendeleo nalo na sasa mifuko ya Saruji"alisema Padre Muyinga
Padre Muyinga aliongeza kuwa atahakikisha mradi huo wa ujenzi wa vyumba vya madarsa sita unaojengwa kwa muundo wa ghorofa unakamilika kwa wakati,ambapo ametenga kila siku ya Jumatano kuwa siku ya kuwaombea wafadhili na watu mbalimbali wanaojitolea kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
Nao baadhi ya wananchi wa kata hiyo akiwamo Maria Sanga na Jackson Kikoti alisema kuwa kijiji hicho kinakabiliwa na changamoto ya maji huku mdau huyo akiahidi kutatua changamoto ya maji siku za karibuni.
Kikoti alisema kuwa wananchi hao hususani kina mama wanatembea umbali mrefu kutafuta maji jambo ambalo linaweza kuhatarisha familiya zao.
0 maoni:
Chapisha Maoni