Posted by Esta Mlaibiche on JULY 31,2017 IN NEWS
Mbunge wa jimbo la Mji wa Kibaha ,Silvestry Koka akieleza maadhimio ya baraza la mji huo yaliyotolewa kwenye baraza la madiwani
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya
Mji wa Kibaha, Lucy Kimoi akizungumza jambo katika baraza la madiwani
la Mji huo .(picha na Mwamvua Mwinyi)
……………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
BARAZA la madiwani la
halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Pwani ,limeadhimia mkuu wa idara ya
mazingira Tumaini Kaila na wa idara ya maji Grace Lyimo wachukuliwe
hatua na mamlaka za ajira zao endapo watabainika kuzembea kusimama
majukumu yao .
Akielezea maadhimio
ya madiwani hao ,mbunge wa jimbo la Mji wa Kibaha ,Silvestry Koka
,alisema baraza hilo pia limemkataa mkuu huyo wa idara ya
mazingira kutokana kukosa ushirikiano na kushindwa kusimamia hali ya
usafi ya mji huo ambayo hairidhishi .
Aidha limeitaka mamlaka husika ya ajira yake imchukulie hatua stahiki kwa mujibu wa ajira yake.
Koka alisema
wameshindwa kumvumilia mkuu huyo wa idara ya mazingira kwani huwezi
kufanyakazi pasipo kuwa na mahusiano mazuri na madiwani wala watendaji
wengine .
“Maeneo mengi na ya
wazi hayapo katika usafi hivyo na hili nalo tumeshapiga kelele
,tumeshauri ,hashauriki ,ni bora mamlaka husika imuwajibishe .” alisema
Koka .
Hata hivyo ,madiwani
hao wameelekeza wakandarasi washauri na wasimamizi wa miradi ya maji
wachukuliwe hatua zile zinazostahiki kwa kushindwa kusimamia miradi hiyo
na kusababisha hasara ya mil.132 .
Walitaka wakandarasi hao wachukuliwe hatua kwa kulingana na mikataba yao.
Koka alibainisha
kwamba ,waajiriwa wa halmashauri waliosimamia miradi ya maji wakiongozwa
na Grace Lyimo ,mamlaka zao zinazowasimamia ziangalie hatua za
kuwachukulia endapo watabainika kufanya uzembe .
Katika hatua nyingine
,mbunge huyo aliishauri halmashauri na watendaji kukamilisha miradi
mbalimbali ambayo ni viporo ikiwemo zahanati na majengo ya madarasa .
Koka alisema miradi hiyo ambayo haijakamilika ikamilishwe kabla ya kuanza mipya ya aina ile ile .
Alielezea kuwa ,haina
budi fedha zinazoingizwa na serikali ikakamilisha miradi lengwa kwa
maslahi ya jamii kuliko kuishia kati huku mwaka wa fedha mwingine
inaanzishwa miradi mingine hivyo kusababisha kuwa na mlundika wa miradi
ya zamani .
Wakati huo huo ,Koka
alisema kwa mujibu wa sheria 0.03 ya mauzo au huduma kwa viwanda au
kampuni hulipia kodi ya mapato kutokana na bidhaa wanazozalisha .
Alisema licha ya
kulipia mapato kisheria lakini inapaswa halmashauri ikaangalia namna ya
kukusanya asilimia kiasi ya mapato kwenye viwanda na makampuni
yanayozunguka mji huo kwa ajili ya kujiongezea mapato .
“Kila anaetoa huduma inatakiwa halmashauri imfikie ili inufaike na wadau wake”alisema Koka .
Nae diwani wa kata ya
Tumbi ,Hemed Chanyika alisema kwa kushindwa kupeleka taarifa za kata za
maji imechangia kukosa zaidi ya sh mil 100 ambazo wahisani walitakiwa
kuchangia kuleta Maji mjini Kibaha .
Awali akiibua hoja
hiyo ya miradi ya maji kusuasua alisema wakandarasi na watendaji husika
wa idara hiyo watafutiwe kazi nyingine .
Chanyika alielezea
wananchi wanataka kuona majibu na matokeo ya miradi inayotekelezwa na
serikali na wahisani hivyo kama haisimamiwi kikamilifu inakatisha tamaa .
” Miradi ya nyuma
tumeshapata hasara yenye zaidi ya mil. 132 na kutoletwa taarifa za kata
tumekosa mil.100 ambazo tungewezeshwa na wahisani”alisisitiza Chanyika.
Diwani wa viti maalum
mjini humo, Selina Wilson ,alizungumzia changamoto ya kusuasua kwa
fedha zinatengwa kwa ajili ya vijana na wanawake .
Alisema katika halmashauri hiyo fedha hizo hazitolewi zote na zinawekwa kidogo .
Selina alieleza ,kwa
mwaka 2015/2016 kati milioni 306 zilizotengwa lakini zilizopelekwa
kwenye vikundi ni milioni 49 pekee,na zilizobaki milioni 256.
Alisema kwa 2016/2017 zimetengwa milioni 391 zilitolewa hadi sasa ni milioni 174.
Selina aliomba halmashauri hiyo itupie macho makundi hayo kwa kuyawezesha kupitia fedha zao zote zinazotengwa bila kuyabania .
Mwenyekiti wa chama
cha mapinduzi (CCM) Mji wa Kibaha,Maulid Bundala alisema licha ya miradi
ya maji kudorora na miradi ya barabara iangaliwe .
Bundala alisema
wakandarasi wa miradi ya miundombinu ya barabara wasimamiwe ili ijengwe
kwa viwango vinavyotakiwa na kumalizwa kwa wakati.
0 maoni:
Chapisha Maoni