Posted by Esta Malibiche on APRIL 4,2017 IN NEWS
Jovina Bujulu –MAELEZO
Ubora na thamani ya lugha ya
Kiswahili duniani unadhihirika kwa kukubalika kwake, hali hii
inayopelekea lugha adhimu ya Kiswahili kuendelea kukua na kutumika
katika nchi mbalimbali duniani kijamii, kiuchumi na hasa kibiashara na
ushirikiano wa kimataifa.
Mchango wa lugha hii inaipa hadhi
kubwa nchi yetu ambayo ni kitovu cha lugha hii inayotumika kama lugha
rasmi ya mawasiliano katika nyanja mbalimbali na pia ndiyo lugha
unganishi inayotumiwa na watu wengi nchini.
Kihistoria, lugha ya Kiswahili
imekuwa na mchango mkubwa kutokana na kutumika katika harakati za
ukombozi na pia kuwaunganisha Watanzania na kuwafanya wawe wamoja.
Mara baada ya Uhuru Tanzania
ilianzisha Baraza la Kiswahili (BAKITA) na kupewa jukumu la kuimarisha
na kueneza lugha hii , pia kuhakikisha inatumika kwa ufasaha pamoja na
kukuza msamiati wake ili iweze kukidhi matumizi yake.
Mwaka 1968, lugha hii ilianza
kutumika kufundishia katika shule za msingi hapa nchini. Hatua hii
ilimaanisha kila mwanafunzi wa shule ya msingi kuifahamu vizuri kwa
kuiandika, kuisoma na kuielewa.
Aidha, historia ya kuikuza na
kuieneza lugha hii imeanzia mbali, mwaka 1962 hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere aliitumia kuhutubia Bunge la Tanganyika, baada ya
utawala wake, Rais aliyemfuatia, Ali Hassan Mwinyi aliendeleza matumizi
ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za mawasiliano.
Naye Rais wa Awamu ya Tatu,
Mhe.Benjamin Mkapa na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete
walifanikisha maendeleo ya lugha hii kwa kuhimiza matumizi fasaha katika
nyanja za elimu, shughuli zote za Serikali, katika shughuli au
mikusanyiko rasmi pamoja na matumizi mengine ya mawasiliano.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
hakikuwa nyuma katika kuhakikisha kinakuza, kinaeneza na kinakifanya
Kiswahili kitambulike zaidi duniani.
Miongoni mwa jitihada hizi ni
pamoja na kuanza kutumia Kiswahili kama lugha rasmi ya mawasiliano
chuoni hapo ili kuipa msukumo kwa wananchi wa mataifa mengine
yanayohitaji kujifunza lugha hii.
Katika kutambua juhudi hizi za
Chuo, Balozi wa kwanza wa Kiswahili Barani Afrika, Mama Salma Kikwete,
hivi karibuni alimkabidhi tuzo ya Kiswahili Makamu Mkuu wa Chuo hicho
Profesa Rwekaza Mkandara, ikiwa ni utambuzi wa mchango wake kwa
kurasimisha lugha hiyo kutumika katika shughuli zote za Chuo na
kitaaluma ikiwemo mikutano ya Baraza la chuo.
Aidha, Mama Salma alitoa wito kwa
taasisi mbalimbali kuwekeza katika kuendeleza lugha Kiswahili ili
kuieneza kibiashara ndani na nje ya Bara la Afrika.
Kutokana na umuhimu wake katika
mawasiliano hivi karibuni Bunge la Shirikisho la Jumuiya ya Afrika
Mashariki limeidhinisha lugha Kiswahili itumike katika mikutano yake ya
Bunge.
Bunge hilo linajumuisha Wabunge
kutoka katika nchi sita za jumuiya hiyo ambazo ni Tanzania, Kenya,
Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini zimepitisha lugha hiyo kutumika
katika nchi zao. Hatua hiyo ni mwanzo mzuri wa kukipaisha Kiswahili
kimataifa.
Ni kutokana na muktadha huo,
baadhi ya wataalamu wa lugha wameishauri Serikali kuanzisha kozi ya
ukalimani katika vyuo vyake ili kuongeza idadi ya wakalimani hapa nchini
hatua ambayo itawaongezea ajira wahitimu wa kozi hiyo.
Hadi sasa inakadiriwa kuwa idadi
ya wakalimani nchini haizidi 20 mbao ndio wanaotoa huduma katika
mikutano mbalimbali ya kimataifa.
Akizungumza jijini Dar es Saaam
hivi karibuni Katibu Mkuu wa Baraza la Kiswahili (BAKITA), Dkt. Selemani
Sewangi alisema kuwa huu ni wakati muafaka kwa Tanzania kuanzisha kozi
hiyo ili kupata wakalimani wa kutosha na wenye weledi, uwezo na maarifa
katika kukalimani lugha ya Kiswahili kwenda lugha nyingine mbalimbali
duniani.
Aliendelea kusema kuwa Tanzania
haina kozi hiyo nyuoni, hivyo uwepo wa wataalamu hao hasa kipindi hiki
ambacho nchi inapokuwa kiuchumi kwa kasi, kazi hiyo itoe mchngo wake
ikizingatiwa sekta ya utalii inaendelea kuimarika na kuwa na ongezeko la
wageni mbalimbali wakiwemo watalii, wawekezaji na wengine hatua ambayo
itakuwa fursa ya kutangaza utajiri na maliasili zilizoko nchini mwetu.
“Kuwa kuna baadhi ya watu ambao
wanatafsiri lugha ya Kiswahili wakidhani wanafanya taaluma ya ukalimani,
jambo ambalo si sahihi kitaaluma, watu hawa hawawezi kupata ajira
kutokana na kukosa vigezo vya elimu rasmi ya ukalimani” alisema Dkt.
Sewangi.
Akifafanua juu ya maana hasa ya
ukalimani Dkt. Sewangi alisema kuna mkanganyiko kati ya kutafsiri na
kukalimani, ambapo alisema kuwa kutafsiri kunaweza kufanywa na mtu
yoyote, lakini kukalimani ni lazima mtu asomee kozi maalumu ili aweze
kutambulika kimataifa.
Katika kuonyesha msisistizo wa
kuhakikisha kuwa Kiswahili kinapaa kimataifa, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa Kiswahili ni
lugha ya Waafrika na inazungumzwa katika nchi nyingi na imekubalika
kutumika katika mikutano ya Umoja wa Afrika, hivyo aliwashauri
Watanzania kuipenda lugha hiyo.
Hivi karibuni Tanzania
ilitembelewa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Haile Mariam Dessalegn
ambapo alisema kuwa nchi yake imekubali kuchagua Chuo Kikuu kimoja ili
lugha ya Kiswahili ifundishwe nchini mwake kwa kuendelea kuimarisha
uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli aliahidi
kupeleka wataalamu wa lugha ya Kiswahili ili wafundishe katika chuo
kitakachoteuliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia kufundisha lugha hiyo.
Kwa kuzingatia umuhimu wa lugha ya
Kiswahili huu ni wakati muafaka kwa watunga Sera, Mamlaka husika na
Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuanzisha kozi ya ukalimani katika
vyuo vyetu ili wahitimu wapate fursa za ajira katika nchi mbalimbali
na hivyo kuzidi kuipa hadhi na kuieneza lugha ya Kiswahili ambayo
inakisiwa kuwa ni lugha ya 10 miongoni mwa lugha 600 zinazozungumzwa
duniani.
0 maoni:
Chapisha Maoni