Posted by Esta Malibiche on APRIL 28,2017 IN NEWS
Na Denis Gondwe
Iringa
Wastani
wa asilimia 60 ya maji yanapotea yanapopita katika mifereji ambayo
haijasakafiwa na kuchangia katika upungufu wa maji kwenye mzunguko wake.
Kauli
hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu baada ya kikosi
kazi namba tatu kukagua mfereji wa asili katika skimu ya umwagiliaji ya
Mkombozi inayohudumia vijiji sita katika kata za Mboliboli na Itunundu katika
tarafa ya Pawaga wilayani Iringa jana alipoongoza kikosi kazi cha kunusuru
ikolojia ya bonde la mto ruaha.
Ayubu
alisema kuwa jitihada zinahitaki kuhifadhi mazingira yanayozunguka skimu ya
umwagiliaji ya mkombozi yenye mfereji wa asili. Aidha, amepiga marufuku
matumizi ya pampu za kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa sababu hakuna
kibali kilichotolewa kwa matumizi ya pampu katika skimu hiyo. “Matumizi ya
pampu ni marufuku kuanzia leo. Pampu zote ziondolewe katika skimu hii kwa
sababu zipo kinyume na sheria” alisisitiza Ayubu.
Ayubu
aliongeza kuwa jamii nzima inategemeana katika uhitaji na matumizi ya maji na
kusisitiza umakini katika matumizi yake. “Sote tunategemeana. Maji yakitoka
hapa yanaenda kuzalisha umeme bwawa la mtera, yakitoka bwawa la mtera yanaenda
kuzalisha umeme Kidatu, yakitoka kidatu yanaenda katika mashamba ya miwa
kilombero” alisema Ayubu.
Wakati
huohuo, mwenyekiti wa kikosi kazi hicho aliwataka wafugaji wenye mifugo mingi
kujipanga kuvuna mifugo yao ili iendane na ukubwa wa ardhi iliyopo. Alisema
kuwa wingi wa mifugo hauendani na tija inayotokana na mifugo hiyo zaidi ya
kusababisha uharibifu wa mazingira.
Nae
wakili wa serikali mkuu Benard Kongola kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya
Mazingira (NEMC) alisema kuwa mwananchi yeyote atakaye kamatwa akijihusisha na
shughuli za kilimo ndani ya eneo la mita 60 kutoka ukingo wa mto ni kosa la
jinai kwa mujibu wa sheria. Aidha, aliwataka wale wote wanaojishughulisha na
kilimo ndani ya eneo hilo kuacha kabla ya zoezi la kuwakamata litakapoanza
baada ya wiki moja.
0 maoni:
Chapisha Maoni