Ijumaa, 28 Aprili 2017

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU SHUGHULI ZA KIBINADAMU KATIKA VYANZO VYA MAJI IRINGA



Posted by Esta Malibiche on APRIL 28,2017 IN NEWS


Na. Dennis Gondwe, Iringa
Serikali mkoani Iringa imepiga marufuku shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji wilayani Iringa ili kunusuru uendelevu wa bonde la mto Ruaha mkuu.
Marufuku hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa kikosi kazi namba tatu cha kunusuru ikolojia ya mto Ruaha mkuu ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu baada ya kukagua chanzo cha maji cha Kivalali kilichopo katika kijiji cha Bandabichi wilayani Iringa katika ziara ya kukagua uharibifu wa vyanzo vya maji katika kata ya Ifunda.
Ayubu alisema “kikosi kazi hiki kimeundwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuangalia njia sahihi ya kuhifadhi ikolojia ya vyanzo vyote vya mto Ruaha mkuu. Baada ya kutembelea vyanzo vya maji, ni kweli shughuli za kibinadamu zinafanyika ndani ya hifadhi ya vyanzo hivyi. Naagiza mazao yote yaliyolimwa ndani ya hifadhi ya maji iliwa ni pamoja na vitindi vya ulazi viondolewe”. Alisema kuwa kikosi kazi hicho kilichoundwa na Jamhuri kina lenga maslahi mapana ya Taifa tofauti na matakwa ya mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu wachache.
Wapo baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kuvamia kidogo kidogo maeneo yenye maslahi ya kitaifa na baadae kujimilikisha wakidhani serikali wanaimiliki wao. Tabia hiyo sasa ifike mwisho, lazima kila mwananchi aheshimu na kufuata sheria na taratibu za nchi kwa ustawi wa taifa zima” alisema Wamoja.
Wakati huohuo, Mkurugenzi mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alishauri eneo lote la mkondo wa maji libainishwe na kupandwa miti ya asili. Alisema kuwa miti hiyo ya asili itasaidia kutambua mipaka ya maeneo ya vyanzo vya maji pamoja na kusaidia uhifadhi wa vyanzo hivyo na kuzuia kuvamiwa kiholela. Alisema kuwa uhifadhi wa vyanzo vya maji utasaidia uendelevu wa shughuli nyingine za kimandeleo kuanzia uhifadhi wa mazingira, wanyama, watumia maji na shughuli za kilimo nchini.

0 maoni:

Chapisha Maoni