Posted by Esta Malibiche on MAY 3,2018 IN NEWS
Na. Atley Kuni OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo ameahidi kuwa shule ya Wasichana Iringa
iliyopo mkoani Iringa itafanyiwa ukarabati ikiwa ni muendelezo wa
serikali katika kuzikarabati shule zake kongwe hapa nchini.
Jafo alitoa kauli hiyo akiwa
njiani kuelekea Dodoma, ambapo ili mlazimu kufanya ziara yakushtukiza
shuleni hapo na kuzungumza pamoja na walimu, watumishi wasio walimu
pamoja na wanafunzi wa shule ya Iringa wasichana kisha kuzulu na
kujionea miundombinu mbalimbali katika shule hiyo iliyo anzishwa toka
mwaka 1967.
Akizungumza mara baada yakuijionea
hali ya miundombinu kwenye shule hiyo, Mhe. Jafo aliiambia jumuiya hiyo
kuwa Shule ya Wasichana Iringa ni miongoni mwa shule kongwe 46 zilizopo
katika mpango wa ukarabati mkubwa kwenye awamu ya pili ili kuwa na
mazingira bora yakusoma na kujifunzia.
“Katika mwaka wa fedha wa 2017/18
tulikarabati shule kongwe 43 na katika mwaka huu wa 2018/19, shule hii
pamoja na zingine kongwe 46 hapa nchini zitakuwa katika mpango kamambe
wa kukarabatiwa kama tulivyokwisha fanya kwenye shule kama 43 za awali
ambapo shule 89 zote kongwe tuwe tumezimaliza” alisema Waziri Jafo.
Sambamba na ukarabati huo Mhe.
Jafo ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zote ambazo ziliainishwa mbele
yake ikiwepo upungufu wa walimu wa Fizikia na Hisabati pamoja na stahiki
za walimu.
“Mama yetu Nkondola, amewasilisha
changamoto za walimu wa Hesabu na Fizikia lakini pia maslahi ya walimu,
naomba niwaahidi kuwa suala hilo nimelichukua lakini niwaahidi kutuma
wataalam kutoka kwenye wizara yangu pamoja na wizara zingine za kisekta
kuja kufanya tathmini ya kina juu ya haya mliyo niambia” alisisitiza
Waziri Jafo.
Mhe. Jafo aliwataka wanafunzi hao
kusoma kwa bidii huku akitoa ahadi mbele ya jumuia hiyo kuwa, endapo
katika mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita watapata daraja la
kwanza (DV.1) zaidi ya watahiniwa 30 wa mwaka huu kwa kidato cha sita
atawandalia sherehe yakujipongeza na wale watakaopata daraja la kwanza
yenye pointi kati ya 3-5 wataalikwa bungeni kwa gharama za Mhe. Waziri
Mhe. Jafo akiwa katika ziara hiyo,
alikagua miundombinu ya shule ikiwapo Mabweni, Vyoo, Bwalo la Chakula,
Jiko na Ofisi za Walimu na kisha kufanya mazungumzo na walimu, watumishi
wasio walimu pamoja na wanafunzi.
Huo umekuwa ni utamaduni wa
kiongozi huyo mwenye dhamana na OR TAMISEMI kila anapopata fursa
kutembelea mikoani kutembelea shughuli za maendeleo kwa wananchi na
sekta zote ili kujionea maendeleo ya watu na shughuli zao.
0 maoni:
Chapisha Maoni