Jumatatu, 14 Mei 2018

DKT. MWIGULU NCHEMBA ATOA AGIZO KWA JESHI LA POLISI NCHINI

Posted by Esta Malibiche on MEI 14,2018 IN NEWS


WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza jeshi la Polisi nchini kuruhusu taasisi za dini kufanya mikutano yao pindi watakapoomba kibali.

Aidha, amesema ni lazima kuheshimu uhuru wa kuabudu wa kila dini uzingatiwe kwa kuruhusu wanafunzi na wafanyakazi kwenda sehemu zao za kuabudu kama ilivyopangwa.

Akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na Kanisa la Waadventista Wasabato jijini Mwanza, Dk Mwigulu alisema kuwa mafundisho yanatotolewa na taasisi za dini yanasaidia kuwa na jamii yenye raia wema.

Alisema kwa kuwa Wizara hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia uhuru wa kuabudu, watahakikisha wanazungumza na mashirika n ahata shule ambazo zinawazuia wanafunzi na wafanyakazi kuhudhuria kwenye ibada siku za jumamosi.

‘’Nimeagiza jeshi la Polisi wawape uhuru wa kuabudu kwa sababu mnatengeneza jamii iliyobora lakini pia tutazungumza na wahusika kwenye taasisi za elimu na ajira ili tutoe maamuzi yatakayotolewa yasilete doa kwani kazi hii inasaidia kunyoosha nchi,’’ alisema Dk Mwigulu.

Naye, Katibu Mkuu wa Kanisa hilo Kanda ya Nyanza Kusini, Steven Swita alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya waumini wa kanisa hilo kuzuiliwa kwenda kuabudu siku ya jumamosi kulingana na imani zao.

‘’Kumekuwa na utaratibu wa kupangwa masomo ya ziada na mitihani siku ya jumamosi pamoja na udahili wa wafanyakazi na wasipohudhuria huadhibiwa kwa viboko kwa wanafunzi wa shule za msingi na wale wa elimu ya juu wanafukuzwa shule,’’ alisema Swita
Alifafanua kuwa wanaamini kuwa kuachishwa kazi au kutengwa kwa waajiriwa na kufukuzwa shule au vyuo kwa sababu ya kutohudhuria siku hiyo, wanaathirika kisaikolojia kwa kushindwa kutimiza ndoto zao.

Alisisitiza kuwa matukio hayo yanapaswa kuangaliwa ili wasikose nafasi ya kutumikia taifa na kuhudhuria ibada zao.

‘’Tunaunga mkono mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ili kuboresha huduma za jamii na kuleta maendeleo kwa taifa, pia tunaheshimu azma ya serikali kudumisha usalama na amani ili wananchi wajipatie maendeleo na kuondokana na maadui watatu,’’ alisema
Pia alisema wanaunga mkono serikali kwa juhudi zinazoendelea na kwamba watafundisha watu kuwa na hofu ya Mungu ili kushiriki katika ujenzi wa Taifa












.

0 maoni:

Chapisha Maoni