Posted by Esta Malibiche on MEI 25,018 IN NEWS
Kujengwa kwa kiwanda hicho kumedhihirisha juhudi za wilaya hiyo chini ya mkuu wake wa wilaya, Asiah Abdalla za kutekeleza kwa vitendo mkakati wa mkoa wa Iringa wa ujenzi wa viwanda 100 ifikapo Desemba mwaka huu.
Ujenzi wa kiwanda hicho kinachojengwa kwa zaidi ya Sh Bilioni 1.7 katika kijiji cha Lundamatwe wilayani humo ulianza Januari mwaka huu.
Akitoa taarifa ya ujenzi kwa kiongozi huyo, mwakilishi wa kampuni ambaye pia ni Afisa Mahusiano na Maendeleo ya Jamii wa kampuni hiyo, Robert Nyachia alisema kukamilika kwa kiwanda hicho kutaifanya kampuni yao iwe na uwezo wa kuzalisha nguzo 180,000 kwa mwaka na kutoa ajira zaidi ya 100 wakati wote wa uzalishaji.
“Lakini pia kitatoa hamasa ya uhifadhi wa mazingira kupitia kilimo cha miti katika maeneo yaliyo wazi ambayo hayatumiki kwa kilimo na ufugaji na kutoa soko la uhakika la miti yote itakayokidhi vigezo vya ubora toka kwa wananchi,” alisema.
Pamoja na ujenzi wa kiwanda hicho, Nyachia alisema kampuni yao ina miliki kisheria shamba la ekari 5,000 za miti wilayani Kilolo ambazo kati yake ekari 2,400 zimepandwa miti aina ya milingoti ambayo ni malighafi ya kuzalisha nguzo na ekari 2,600 za miti aina ya misindano.
Kwa ufadhili wa serikali ya Finland na Mfuko wa Misitu Tanzania, alisema kampuni hiyo imewawezesha pia wakulima zaidi ya 1,200 kupanda miti zaidi ya 2,400,000 wilayani humo.
Akizungumzia mahusiano ya kampuni na jamii inayozunguka miradi yao, alisema kampuni imetumia zaidi ya Sh Bilioni 2.2 kuchangia shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii ya wilaya hiyo.
Alitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati tatu, nyumba mbili za waganga, nyumba moja ya mwalimu, wodi ya wajawazito na wagonjwa, vyumba vinne vya madarasa, mabweni ya wasichana na ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule mbalimbali za msingi za wilaya hiyo.
Akiipongeza kampuni hiyo, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru aliwataka wazalishaji wa nguzo hizo nchini kuzalisha kwa wingi ili kufikia mahitaji ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
“Nchi ina malighafi za kutosha ambayo ni miti ya kuwezesha uzalishaji wa nguzo hizo kwa wingi. Serikali haina sababu ya kuagiza nguzo toka nje ya nchi kama viwanda vya ndani vinaweza kukidhi mahitaji ya soko kubwa la Tanesco na masoko mengine,” Kabeho alisema.
Taarifa ya Tanesco iliyotolewa mjini Iringa mwaka jana na Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji wa Huduma kwa Wateja, Joyce Ngayhoma inaonesha Tanesco pekee yake inahitaji nguzo zaidi ya 500,000 kila mwaka, kiasi ambacho soko la ndani limeshindwa kutosheleza.
“Kuna wakati tulilazimika kuagiza nguzo kutoka nje ya nchi kwasababu ya changamoto hiyo; wito wetu kwa wazalishaji wa ndani, waongeze uzalishaji ili kutosheleza mahitaji na wazingatie ubora unaotakiwa na shirika,” alisema.
Alisema shirika limejiwekea lengo la kuunganisha wateja wapya zaidi ya 250,000 kila mwaka na kwa hesabu hiyo mahitaji ni makubwa kwasababu wengine wanahitaji nguzo zaidi ya moja ili wafikiwe na huduma.
“Na ikumbukwe tumeingia awamu ya tatu ya miradi ya REA, lengo la serikali ni kuona ifikapo mwaka 2025 vijiji vyote nchini vinakuwa na umeme,” alisema
0 maoni:
Chapisha Maoni