Posted by Esta Malibiche on July 10,2018 IN NEWS
Meneja Miradi wa Taasisi ya Mo Dewji, Rachel Chengula akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada wa Tsh. 125 Milioni kwa kituo cha Tumaini la Maisha kilichopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambazo zitatumika kugharamia matibabu ya watoto wenye saratani.
Baadhi ya watoto ambao wanapatiwa matibabu katika kituo cha Tumaini la Maisha kilichopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
TAASISI ya Mo Dewji imetoa msaada wa Tsh. 125
Milioni kwa kituo cha Tumaini la Maisha kilichopo katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, ili kusaida kugharamia matibabu ya magonjwa ya saratani kwa watoto
wanaopatiwa huduma katika kituo hicho.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Meneja Miradi wa Taasisi ya Mo Dewji,
Rachel Chengula alisema msaada huo ni mwendelezo wa misaada ambayo imekuwa
ikitolewa na taasisi kwa kituo hicho.
Alisema wanatambua hali ngumu ambayo wanapitia watoto hao
wanapouguza magonjwa ya saratani, hivyo wanaamini msaada huo utasaidia
kuboresha huduma kwa watoto waliopo kituoni hapo na kuwezesha watoto waliopo
mikoani kusafirishwa ili kufikishwa hospitalini na wao wapatiwe matibabu.
“Kama upo hai na mwanao anapumua, mshukuru Mungu kuwa ana makusudi
na wewe na ana makusudi na mtoto wako. Usikatishwe tamaa na magonjwa, tunaamini
kwamba watoto hawa watapona na kurudi nyumbani, watasoma na watalitumikia Taifa
letu,
“Kama mnavyofahamu Mohammed Dewji amekuwa akifanya kazi na Tumaini
la Maisha tangu mwaka 2012 ili kusaidia watoto kupatiwa matibabu, na kupitia
taasisi yake tutaendelea kushirikiana ili kusaidia watoto wetu wapatiwe
matibabu,” alisema Chengula.
Naye Meneja wa Wafadhili wa kituo cha Tumaini la Maisha, Alex
Kaijage aliishukuru Taasisi ya Mo Dewji kwa msaada ambao wamekuwa wakiwapatia
na kuwaomba kuendelea kuwa na moyo huo wa kusaidia matibabu ya watoto wenye
saratani ili warejee katika hali ya kawaida na kuendelea na shughuli zingine
ikiwepo kusoma.
“Tunajua kwamba tunahitaji sana sana hizi fedha kufanikisha
matibabu ya hawa watoto, sio tu usafiri wa kutoka huko wanakotoka na kuja bali
hata dawa ambazo tunazipata kwa sababu ya huu mchango ambao Mohammed Dewji
ametuwezesha. Kwa sababu yenu watoto hawa wanapata matibabu, kwa sababu yenu
wanapona kwahiyo tunawashukuru sana,” alisema Kaijage.
Kwa upande wa mmoja wa wazazi ambao mtoto wake anapatiwa matibabu
katika hicho, Hamisi Samweli aliwataka wadau wengine wenye uwezo wa kifedha
kuwa na moyo wa kusaidia kama anavyofanya Mohammed Dewji ili watoto ambao
wazazi wao hawana uwezo wa kifedha wapatiwe matibabu.
0 maoni:
Chapisha Maoni