Kwa Habari za kitaifa na kimataifa

Tembelea Kali ya habari

Kwa habari za michezo na burudani

Tembelea Kali ya habari

Kwa habari za afya

Tembelea Kali ya habari

Kwa habari za Kilimo

Tembelea Kali ya habari

Kwa habari za uchumi na biashara

Tembelea Kali ya habari

Kwa habari za elimu

Tembelea Kali ya habari

Jumanne, 31 Mei 2016

Serikali yaanza kutumia TEHAMA Kuendesha mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma.

mae1Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira Bi. Riziki Abraham (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari Leo jijini Dar es salaam kuhusu utaratibu mpya wa kutumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutangaza nafasi za kazi,kupokea maombi,kuwaita kwenye usaili waombaji wa kazi na kuwapa  taarifa za kazi na kuwawezesha waombaji kupata ajira kwa kutumia mfumo huo (TEHAMA).Kulia ni Kaimu Naibu Katibu wa Sekretarieti hiyo anayeshughulikia TEHAMA Bi. Mtage Ugullum.
mae2Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Ofisi ya Rais  Sekretarieti ya Ajira uliofanyika leo jijini Dar es salaam Ukilenga kutoa taarifa kuhusu matumizi ya  teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuendesha mchakato wa ajira katika utumishi wa umma.
(Picha na Idara ya Habari Maelezo)
……………………………………………………………………………………………………..
Frank Mvungi-Maelezo.
Serikali imeanza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA) katika kutangaza nafasi za kazi,kupokea maombi,kuwaita waombaji kazi kwenye usaili na kuwawezesha kutumia teknolojia hiyo kupata ajira.
 Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira Bi Riziki Abraham wakati wa mkutano na Vyombo vya Habari uliolenga kueleza mikakati ya Serikali kuboresha mfumo wa kupokea maombi ya ajira  na kuyashughulikia.
 “Sekretarieti ya Ajira inatoa rai kwa waombaji fursa za Ajira kujisajili katika mfumo wa Ajira unaopatikana kupitia anuani ya tovuti ya www.ajira.go.tz na mfumo wa” job alert system” au kupitia simu za kiganjani kwa kupiga *152*00# ili kuomba fursa za ajira zinazopatikana” Alisisitiza Riziki.
Akifafanua kuhusu faida za kutumia TEHAMA kuendesha mchakato wa ajira, Riziki amesema kuwa mfumo huo unasaidia kupunguza idadi ya siku za kuendesha mchakato wa ajira kutoka siku 90 hadi 52 kwa sasa.
Aliongeza faida nyingine kuwa ni Serikali inapanua wigo wa utoaji taarifa za uwepo wa fursa za Ajira hasa kwa waombaji wa ajira waishio vijijini.
Alisema mfumo huu unalenga kupunguza changamoto kadhaa zikiwemo malalamiko ya baadhi ya waombaji fursa za ajira kuhusu upotevu wa maombi yao ya kazi.
Hadi kufikia Mei, 2016 jumla ya waombaji wa fursa za Ajira waliokuwa wamejiandikisha kwenye mfumo wa utumaji maombi ya kazi walikuwa (97,765).
Aidha jumla ya waombaji wa fursa za Ajira 89,484 wamejiunga kwenye mfumo wa kupata taarifa za uwepo wa fursa za Ajira kupitia simu za kiganjani.

ZIARA YA RAIS KUTEMBELA SEHEMU ZILIZOHARIBIWA NA WAPINZANI (CUF)

zi1Wanachama cha Mapinduzi CCM Tawi la Tibirinzi Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba wakimasikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein (hayupo pichani) wakati alipotembelea tawi lao lililochomwa moto na Wapinzani kwa sababu za kisiasa kuona hali ya uharibifu uliotokea, [Picha na Ikulu.] 31/05/2016.
zi5Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein akisalimianana Sheha wa Shehia ya Maziwa Ngombe Bi,Asha Yussuf Hassan, aliyevunjiwa Nyumba yake na Wafuasi wa Chama cha CUF hivi karibuni kwa sababu za kisiasa pamoja na kukatiwa Migomba yeke wakati alipomtembelea leo kuangalia maafa hayo, [Picha na Ikulu.]31/05/2016.
zi6Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein akisalimianana Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Micheweni wakati alipomtembea Sheha wa Shehia ya Maziwa Ngombe Bi,Asha Yussuf Hassan, aliyevunjiwa Nyumba yake na Wafuasi wa Chama cha CUF hivi karibuni kwa sababu za kisiasa pamoja na kukatiwa Migomba yeke wakati alipomtembelea leo kuangalia maafa hayo, [Picha na Ikulu.]31/05/2016.
zi7Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein (wa pili kulia) akipata maelezo ya ushuhuda kutoka kwa Sheha wa Shehia ya Maziwa Ngombe wilaya ya Micheweni Pemba, Bi,Asha Yussuf Hassan (katikati) aliyevunjiwa Nyumba yake na Wafuasi wa Chama cha CUF hivi karibuni kwa sababu za kisiasa pamoja na kukatiwa Migomba yeke wakati alipomtembelea leo kuangalia maafa hayo, [Picha na Ikulu.]31/05/2016.
zi8Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein akizungumza na wanachama cha Mapinduzi Tawi la Tibirinzi Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba ambalo lilichomwa Moto na wapinzani  hivi karibuni,akiwa katika ziara maalum ya kutembelea maeneo mbali mbali yaliyopata matukio ya kisiasa,[Picha na Ikulu.] 31/05/2016.
zi2Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein (wa pili kulia) alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Shehia ya Maziwa Ngombe wilaya ya Micheweni Pemba leo wakati alipomtembelea Sheha wa Shehia hiyo Bi,Asha Yussuf Hassan (katikati) aliyevunjiwa Nyumba yake na Wafuasi wa Chamacha CUF hivi karibuni kwa sababu za kisiasa pamoja na kukata Migomba yeke, [Picha na Ikulu.]31/05/2016.
zi3Mkuu wa Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe,Rasshid Hadid (wa pili kulia) akitoa maelezo kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein (katikati) wakati alipofika Kijiji cha Shengejuu shehia ya Pembeni kutembelea ujenzi wa Nyumba ya Nd,Said Khamis Iliyobomolewa na Wafuasi wa Chama cha CUF kwasababu za Kisiasa,(kushoto) Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mhe,Vuai Ali Vuai,[Picha na Ikulu.]31/05/2016.

TANROADS yakanusha kudaiwa fidia

3Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wamekanusha kudaiwa fidia na wananchi wa Kijiji cha Mazingira,Wilaya ya Handeni mkoani Tanga waliovunjiwa nyumba zao ili kupisha ujenzi wa barabara.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Meneja wa TANROADS Mhandisi Alfred Ndumbaro alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii juu ya malalamiko ya wananchi wa Kijiji hicho kuhusu kutolipwa fidia zao.
”Sheria iko wazi kuwa wanaojenga karibu na barabara wakivunjiwa hawalipwi fidia yoyote lakini wale ambao ujenzi wa barabara uliwafuata katika maeneo yao wana haki ya kulipwa fidia”, alisema Mhandisi Ndumbaro.
Mhandisi Ndumbaro ameongeza kuwa zoezi la malipo ya fidia kwa wanakijiji waliokuwa na uhalali wa malipo hayo lilishakwisha zamani kwa hiyo, wanaodai sasa ni wale ambao nyumba zao zilivunjwa kutokana na kujenga eneo la barabara.
Aidha, Mhandisi huyo ametoa rai kwa wananchi kufuata sheria za ardhi ili kupata uhalali wa viwanja vyao pamoja na kuepuka usumbufu na gharama za kuvunjiwa nyumba zao.
Nyumba hizo zilivunjwa ili kupisha ujenzi wa barabara ya lami yenye Kilomita 54 kutoka Mkata hadi Handeni iliyojengwa na Kampuni ya Synohydro Corporation Limited ya China.

WAZIRI WA AFYA MHE.UMMY MWALIMU ATOA TAMKO KUHUSU SIKU YA KUPINGA MATUMIZI YA TUMBAKU DUNIANI, TAREHE 31 MEI 2016


imagesSiku ya kupinga matumizi ya Tumbaku Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 31 Mei.
Kaulimbiu  ya  Maadhimisho ya  Siku ya kupinga matumizi ya tumbaku mwaka 2016 ni “jiandae kwa pakiti zisizo na matangazo wala vivutio”
Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha jamii juu ya kujiepusha au kujikinga na vivutio mbalimbali vya matangazo yanayo hamasisha matumizi ya sigara ambayo ina madhara mengi kiafya.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inaadhimisha siku hii, kwa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na matumizi ya sigara na bidhaa za tumbaku.
Tafiti nyingi zinathibitisha madhara yatokanayo na matumizi ya tumbaku ni pamoja na magonjwa yasiyoambukiza  kama vile saratani, magonjwa ya mishipa ya damu na moyo, kiharusi, magonjwa ya njia ya hewa.
Tafiti pia zinaonyesha takriban watu 6,000,000 hupoteza maisha duniani kwa mwaka kwa utumiaji wa tumbaku na bidhaa zake.
 
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani kwa mwaka 2016, inalenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya tumbaku na kusisitiza kwa wazalishaji kutokuweka maandishi au nembo zinazovutia ili kuishawishi jamii kutumia bidhaa hizo. Aidha tumbaku imekuwa ikisababisha madhara kiafya kama vile magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza. Magonjwa hayo ni magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani, ugonjwa wa kisukari na magonjwa ya njia ya hewa.
Mambo mengine yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kupita kiasi, kutofanya mazoezi, unywaji pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.
Ili kuzuia maradhi yasiyoambukiza yatokanayo na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni kutovuta sigara na kama wewe ni mvutaji, kutovuta sigara hadharani maana madhara yake ni sawa hata kwa mtu asiyevuta ambaye anapata moshi kutoka kwa mvutaji, kuendelea kuielimisha jamii juu ya madhara mbalimbali yatokanayo na utumiaji wa tumbaku hususani kwa vijana.
Serikali inaendelea na mkakati wa tiba kwa watu wenye uraibu wa  matumizi ya tumbaku, ikiwa na lengo kupunguza matumizi hayo miongoni mwa jamii. Kuhakikisha pakiti za tumbaku na bidhaa zake ziwe na tahadhari ya madhara ya utumiaji wa tumbaku na bidhaa zake. Aidha, serikali, inaendelea kurekebisha sheria, kanuni na taratibu za udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatumia  maadhimisho   haya kuwa sehemu ya uhamasishaji kwa jamii kama ilivyo kwenye nchi zote duniani.

SERIKALI YAITAKA RITA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI KUHUSU UMUHIMU KUANDIKA WOSIA WA MIRATHI

indexNa Mahmoud Ahmad Arusha.
SERIKALI imeitaka wakala wa usajili,Ufilisi na Udhamini, RITA, kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuelewa umuhimu wa kuandika wosia na mirathi ,ili kuondoa migogoro kwa familia wakati wa kugawa mirathi ya marehemu.
Rai hiyo imetolewa jana na mkuu wa wilaya ya Arusha, Fadhili Nkurlu, alipokuwa akifungua kampeni ya siku NNe ya kisheria inayotolewa bure na RITA, kuhusu kuandika mirathi na wosia na kuwaelekeza eneo salama la kuhifadhi wosia ukisha andikwa na mhusika   ili kuondoa migogoro mingi kwa familia pindi mhusika anapofariki dunia.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema,wananchi wengi hawana elimu juu ya wosia na mirathi hivyo RITA, ambayo ni wakala wa  serikali ina jukumu kubwa la kuhakikisha elimu inawafikia wengi na hivyo kuwezesha wajane na watoto ambao ndio waathirika  kupata mirathi .
Alisema wosia unasaidia kutatua migogoro ambayo ingelijitokeza wakati wa kugawa mirathi ya marehemu na mtu kuandika wosia sio uchuro bali ni kuweka utaratibu wa mali za muhusika zitakavyogawiwa pindi akisha fariki dunia.
Aliikumbusha jamii kuwa msimamizi wa mirathi sio mrithi wa mali ya marehemu bali jukumuake ni kukusanya mali yote na madeni yote ya marehemu na kusimamia ugawaji na ulipaji wake na kamwe msimamizi yeyote asijihusishe na urithi .
Jamii nyingi zimekuwa zikiingia kwenye migogoro ya kugawana mirathi kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha ya kuandika wosia  kabla ya kifo na matokeo yake wanaoathirika ni wajane na watoto ambao hukosa haki yao .
Awali mratibu wa kampeni hiyo,msajili na wosia kutoka makao makuu ya RITA, Augostino Mbuya, alisema migogoro mingi imekuwa ikijitokeza kwenye familia wakati wa kugawa mirathi kutokana na kutokuwepo kwa wosia ambao ni mwongozo wa jinsi ya kuigawa mali ya marehemu kwa wahusika na matokeo yake watoto na wajane hukosa haki yao ya kurithi.
Alisema kutokana na hali hiyo RITA, ipo tayari kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma hiyo ya kuandika wosia kutokana na wananchi wengi kutokuwa na elimu na kufahamu wapi watapata huduma hiyo ya kuandika wosia na ugawaji wa  mirathi za marehemu
Mbuya,alisema mkakati uliopo ni kusogeza huduma ya kuandika wosia na mirathi ngazi za mikoa na wilaya pamoja na kuhakikisha wanakuwepo wanasheria wa kutosha lengo ni kuiwezesha jamii kuondokana na migogoro ambayo inaweza kuepukwa wakati wa kugawa mali za marehemu.
Alisema tangia kuanzishwa kwa huduma hiyo ya Rita, imeweza kusajili wosia zaidi ya 300 na 30 kati yake zimeshachukuliwakwa  utekelezaji .
Akisoma taarifa ya kazi za Rita, msajili wa mirathi na wosia, kutoka makao makuu ya Rita, Joseph Mwakatobe amesema mahakama kuu imeiteua RITA, kusimamia utatuzi wa migogoro  ya urithi na uandishi wa wosia lngo ni kuondoa migogoro inayojitokeza pindi mtu anaofariki dunia.
Alisema Rita, itaendesha kampeni hiyo ya kuhamasisha wananchi kuhusu kuandika mirathi na wosia katika mkoa wote wa Arusha,ili kuwezesha wajane na watoto wanapata haki yao ya kurithi mali za marehemu .
Aliongeza kuwa kuandka wosia ni swala lahiari ya mtu,na Rita, imekuwa ikikumbana na changamoto mbaimbali zkiwemo za kutokuwepo na wosia wakati wa mirathi .
Aliongeza kuwa mirathi inatolewa kulingana na sheria za dini ya kiislamu, mila na sheria ya India ya mwaka 1865 ambayo inahusisha makundi yote ambayo hayapo kwenye makundi ya kidini na mila.

SERIKALI ITAHAKIKISHA INAENDELEA KULINDA RASILIMALI ZA NCHI IKIWEMO URITHI WA DUNIA

 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa
…………………………………………………………………………………………….. 
Woinde shizza,Arusha

SERIKALI ya awamu ya tano  imesema kuwa itaendeleza jitihada za
kutunza na kulinda urithi wa dunia ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi
wanaoishi maeneo ya uhifadhi ili watanzania wote waweze kunufaikana
rasilimali za nchi .



Hayo yalisemwa na  waziri mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akifungua
mkutano wa kulinda urithi wa dunia wa Afrika kama nyenzo ya maendeleo
endelevu unaoendelea jijini Arusha


Majaliwa alisema kuwa rasilimali zilizopo ni za watanzania na ili
kuhakikisha kuwa wananufaika nazo serikali itahakikisha  inatunza na
kulinda uhifadhi ili yawe endelevu na  kusaidia vizazi vijavyo.


Alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi tajiri yenye urithi na hivyo ili
kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika haswa waishio maeneo ya uhifadhi
serikali itatoa elimu ya kutosha ili waepuke kuchangia uharibifu wa mazingira
unaotokea kwenye hifadhi za taifa .

“Rasilimali hizi ni zetu na hivyo hata wanaoishi maeneo ya hifadhi
watusaidie kwa wale wanaoingilia na kuharibu  kwani hata hizo mali
asili zinatusaidia sote na ndiyo sababu  tumewekea mikakati ya kutunza maeneo
hayo ili yawe endelevu’alisema


Kwa upande wake mwenyekiti wa mkutano huo ambaye ni Katibu Mkuu Wizara
ya Mali asili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi Alisema kuwa
madhumuni ya mkutano huo ni kutambua changamoto na mambo ambayo
yanatishia  na kuathiri uhifadhi bora wa maeneo ya urithi wa dunia
katika afrika .


Aidha mkutano huo utapendekeza suluhisho kwa kupitia upya shughuli
zinazotekelezwa katika eneo la urithi wa dunia na kuangalia mchango wa
miradi ya jamii za kiafrika na kuandaa muelekeo wa miaka kumi ijayo.


Milanzi alisema kuwa mkutano huo utapendekeza suluhisho kwa kushawishi
wanawake kuongeza ushiriki wao katika miradi inayoendana na uhifadhi
wa urithi na maendeleo endelevu pamoja kuchunguza jinsi mitafaruku
inayotokea kwenye maeneo ya urithi wa dunia  kutokana na makundi ya
kigaidi na kutunza amani utamaduni na uridhi asilia.


Aliongeza kuwa pia  mkutano huo umejikita kwenye sera ya UNESCO  ya
mwaka 2015 inayohusu kujumuisha maendeleo endelevu kwenye mkataba wa
uridhi wa dunia.


“mkutano huo pamoja na matokeao tegemewa kisayansi, pia utakuwa na
manufaa kwa taifa na sio tu kuitangaza Tanzania kutalii na kisasa bali
pia ni fursa muhimu ya kiuchumi kutokana na idadi ya wageni watakao
huthudhuria  mkutano huu pamoja na kuanzisha mitandao wa kitaaluma na
kujenga mitaji wa kijamii”alisema Malinzi


Aidha pia mara baada ya mkutano huu na kupata muafaka wa yote kutakuwa
na tamko lililotokana na majadiliano yaliyokuwa yakifanyika siku zote
za mkutano na tamko hili linatarajiwa kutolewa katika hifadhi ya taifa
ya Ngorongoro

Zanzibar yaadhimisha siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani

indexMwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Zanzibar Dkt. Ghirmany akitoa taarifa ya Shirika hilo kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Wizara ya Afya Zanzibar.
Picha Na Miza Othman – Maelezo Zanzibar.
………………………………………………………………………………………………….
Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar
Inakadiriwa zaidi ya watu milioni sita duniani kote hupoteza maisha kila mwaka kutokana na athari za matumizi ya tumbaku na wanaoathirika zaidi ni vijana wenye umri wa miaka 30 hadi 39.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Wizara ya Afya kwenye maadhimisho ya siku ya kupinga  matumizi ya tumbaku Duniani, Meneja wa Kitengo  cha maradhi yasiyoambukiza Zanzibar ndugu Omar Mwalimu Omar amesema mbali na kusababisha vifo, matumizi ya tumbaku yamekuwa chanzo kikubwa cha maradhi.
Amesema tafiti zilizofanyika zimeonyesha kuwa matumizi ya tumbaku yanachangia kwa asilimia 71 kupata saratani ya mapafu, asilimia 42 magonjwa ya njia za hewa na asilimia kumi magonjwa ya moyo.
Ndugu Omar amesema pamoja na kuwa Zanzibar haizalishi tumbaku na haina viwanda vya sigara, bado matumizi ya bidhaa hizo ni ya kiwango cha juu.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2011ulionyesha asilimia 7.3 ya wazanzibari kati ya miaka 25 hadi 64 ni watumiaji wa sigara na asilimia 4.1 wanatumia tumbaku kwa njia za kunusa na kuvuwata.
Meneja wa Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza amezitaja athari nyengine zinazotokana na matumizi ya tumbaku ni kuanguka kwa uchumi wa nchi.
“Kama nilivyotangulia kusema, rika linaloathirika zaidi ni vijana wa miaka 30 hadi 39 ni wazi kuwa nchi zinapoteza nguvu kazi ambayo ipo katika umri wa kuongeza kipato cha nchi,” alisisitiza Ndugu Omar.
Amekiri kuwa katika vita vya kupambana na matumizi ya tumbaku kumejitokeza changamoto ya viwanda vinavyotengeneza bidhaa za tumbaku kuwa na nguvu kubwa ya kifedha na matumizi ya tumbaku imekuwa moja kati ya starehe hususan katika jamii ya vijana.
Amewataka waandishi wa habari kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Wizara ya Afya ya kudhibiti  matumizi ya tumbaku kwa kuitanabahisha jamii juu ya athari zinazotokana na tumbaku.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) aliepo Zanzibar Dkt. Ghirmany amesema Umoja wa Mataifa umepanga kila ifikapo tarehe 31 Mei ya kila mwaka iwe ni siku ya kupinga matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku ili kuitanabahisha jamii juu ya athari inayotokana na tumbaku.
Ameishauri Serikali kuandaa kanuni ya matumizi ya tumbaku ili sheria iliyotungwa ya kudhibiti uvutaji wa sigara katika maeneo ya wazi iweze kufanya kazi.
Ujumbe wa mwaka huu katika kuadhimisha siku ya kupinga  matumizi ya tumbaku Duniani ni ‘kuwa tayari kuondosha  vivutio katika paketi za kuhifadhia sigara’.